Thursday, April 30, 2009

Kama zipo jenga hata 'mbinguni'


Majumba ya 'wakubwa' juu ya mawe, huko Kapri Point jijini Mwanza. Wenzao waliojenga ovyo huko milimani wanaulizwa vyoo; je, hawa vyoo vyao viko wapi?

Sekondari Kamachumu


Hata hizi shule zenye majina kuna siku zilianza kama hii ya kata Kamachumu huko Kagera.

Hawa ni wanafunzi wa kwanza wa kidato cha kwanza mwaka 2009 na mwalimu wao aitwaye Mwesiga Nduba. Hakika wanayo safari ndefu.

Yaliyojiri Kwenye Mabomu Dar

Majeruhi akiwahishwa hospitali

Hata wanajeshi waliumia katika sekeseke hilo

Hata sisi haya hatuyafyatua siku nyingi



Ngoja nitimue mbio, hali haijatulia



Hakuna magari lakini lazima tuhame Mbagala





Njoo mzime moto nyumba yangu inateketea, jamani...haya nenda tu huko jeshini sisi tufe





Bomu limechimba shimo likajifukia lenyewe humu





Wednesday, April 29, 2009

Hali sasa Tulivu-Lukuvi

Wananachi wakiangalia mabaki ya mojawapo ya mabomu yaliyoruka umbali wa km4. Ni moja ya takriban ya mabomu 12 yaliyolipuka na kutua uraiani...

Taarifa zilizotufikia muida huu na kukaririwa na Globu ya Jamii ,Mkuu wa Mkoa wa Dar, William Lukuvi, hali kwa sasa ni shwari na wadau wanaweza kurejea majumbani mwao.
Zaidi ni kwamba, majeruhi wengi wamepelekwa hospitali ya Temeke wengine Muhimbili, inasemekana watu takriban 100 wamejeruhiwa. Aidha, majengo ya shule ya St. Anthony yaliathirika kwani vioo vya madirisha karibu yote yamevunjika, na nyumba kibao zimeharibika.

Kesi ya Kufuru

Yusuf Manji (pichani), yule aliyetajwa na Reginald Mengi kama fisadi papa amefungua kesi ya kashfa, akimtaka Mengi amlipe Sh 1 (moja) kama fidia.
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupitia kwa kampuni ya uwakili ya Muganda, Kamugisha na Bwana, lengo likiwa kutaka kusafishwa. Wengi wameipa tafsiri tofauti kesi hiyo; je, Sh 1 ndiyo thamani ya Manji; je, Mengi hana uwezo wa kumfidia Manji; au, Manji hana shida na pesa, bali kusafishwa.

Mbagala: Hii kali zaidi


Vijana hawa walikamatwa maeneo hayo wakijisevia makasha haya kwa kudhani ni kuwa ni dili kwao na hasa ikizingatiwa biashara ya vyuma chakavu ilivyoshamili hapa Bongo Hii ni kwa mujibu wa Bongopicha. Tahadhari iliyotolewa na jeshi katika eneo la tukio ni kuwa, bomu ambalo wanashughulikia lisilipuke ni athali zinazofikia umbali wa km40. Mabomu mengi yamerushwa na kuangukia katika makazi ya watu, baadhi yametoa umbali hadi wa km6, mf eneo la Kurasini, Yombo, Maji matitu na Polisi Ufundi.

Mwingine karipoti haya: Ninaavyoandika kaka mmoja ananipa taarifa huko Temeke Hospital nakofull....watu wanalia na kuna watoto waalioamua kukimbia wamepotea nakama kuna mtu utamwona mtoto amevaa nguo ya shule imeandikwa mbagala kwa nyuma wengi walivaa tshirt jaribu kumsaidia yawezekana hata nauli hawana wengine wameacha mabegi....cha kusikitisha vibaka wanachambua mali za watu kama hawana akili nzuri huko mbagala.....

Waziri Atuma Rambirambi Mbagala

Kwa niaba ya mbunge mwenzangu wa Kigamboni, na kwa niaba yangu mimi binafsi na wananchi wa jimbo langu la Ukonga, natoa rambirambi na pole nyingi kwa waathirika wa milipuko hii huko Mbagala!
Eneo hilo pia ni jirani yangu kwa upande wa chamazi na kata yangu ya msongola. Nafuatilia sana tukio hili kupitia mtandao huu (Bidii) nikiwa huku Musoma kwenye msiba wa ndugu yangu. Asanteni kwa kuendelea kutuelewesha matukio kama haya.

Mhe. Dr. Makongoro Mahanga
Mbunge wa Ukonga.

Tahadhari Kali Zaidi


Wakubwa, hadi sasa kuna taarifa mtandaoni kuwa watu kumi wameshapoteza maisha kwamshitukon na nyumba kadhaa zinaendelea kulipuka kwa mabomu kwaniyanaangukia kwenye mapaa ya nyumba hizo. Watu wote wanashauri kutokakabisa maeneo hayo.

Lakini Kamanda Kova kathibitisha vifo vya watu wawili tu. Jamani hali ni mbaya sana Mbagala yote nyeupe watu wamekimbia kabisa makazi yao. Waziri wa Ulinzi amedai kuna uwezekano wa mabomu mengine kuendeleakulipuka na kuleta madhara makubwa zaidi. Wameambieni watanzaniawenzetu waliohuko kama bado wapo wasikaribie maeneo hayo kabisa.

Pia, kuna mtu amenasa mawasiliano ya polisi wakielekezana kuwaeleza wafanyakazi walioko kwenye maghorofa jijini kurejea makwao, kwani mambomu makubwa zaidi (kama haya kwenye picha) yakilipuka inaweza kuwa kizaazaa. Magari Kibao ya jeshi yameelekea Mbagala.


Naendelea kufuatilia...

Milipuko ya Mabomu Dar. Duh!




Breaking News...
Huko Mbagala jijini Dar es Salaam ni kimuhemuhe, inasemekana ghala la silaha limeteketea kwenye kambi ya jeshi na mambomu kutikisa jiji zima. Habari zilizotufikia, zikakaririwa na Mzee wa Mshitu aliyeko kwenye chungu cha news, zinasema kuwa nyumba kadhaa zimeungua moto, mtu mmoja kufa na wengine kibao kujeruhiwa kutokana na mlipuko mkubwa wa mabomu umetokea katika jiji la Dar es salaam katika eneo la jeshi Mbagala Kizuiani.

Kwenye mtandao wa Bidii habari ndiyo hiyo: Hali si shwari. Kuna hali ya hofu kwa wazazi wenye watoto wao maeneoyale (shuleni) ambao wanatafuta kila namna ya kupata watoto wao nahawapatikani.Red Cross ndo wanawasili sasa hivi. Kuna bomu ambalo linaelekea kulipuka muda wowote kuanzia sasa. Motounaendelea kuwaka tena kwa kasi kubwa zaidi.Kama ulivyosikia Waziri akitangaza, mlio kwenye majengo marefu Darmkae mkao wa kukimbizana likilipuka lile linalohofiwa."

Mwingine kaandika hivi kwenye Bidii:Nipo hapa office za zantel,milipoko hiyo imesababisha watu wote kutoka nje kutona na mtikisiko mkubwa uliotokea karibu mara mbili hivi.Mlipoko huo umesababisha kuvunjika baadhi ya vitu, vitu hivyo zikiwemo laptop mbili za wateja ambao walikuja kupata huduma ya kuunganishwa na mtandao.

Habari zaidi fuatilia hapa...

Tuesday, April 28, 2009

Mtwara-Mwanza Kwa Taxi

Kwa maeneo mengi katika 'barabara ya John Magufuli' kutoka Mtwara hadi Mwanza mambo ni mswanu (safi) baada aya kukamilika kwa kiwango cha lami; lakini eneo hili pekee (picha ya chini)bado ni korofi hapo Manyoni zapata km100 na kitu hivi, huku kukiwa na matumaini kwa vile mkandarasi anaendelea na kazi.
Ikikamilika, ndoto za John Magufuli za kusafiri kwa taksi kutoka Mtwara hadi Mwanza zinaweza kuwa kweli.

Tuombe Likamilike Rugambwa Azikwe

Sehemu ya Mbele ya Kanisa Kuu (Cathedral) la Katoliki Jimbo la Bukoba linaloendelea kufanyiwa ukarabati wa muda mreeeefuuuu!
Upande wa Mashariki wa Kanisa hilo: Ndani ya Kanisa hilo ndimo aliyekuwa Kardinali wa Kwanza wa Mwafrika, Laurean Rugambwa alitaka azikwe, lakini wakati wa kifo chake, Desemba 8, 1997 lilikuwa linafanyiwa ukarabati, hivyo wahusika wakaamua kuupumzisha mwili wake kwenye Kanisa jingine la Kashozi, lililopo Km 15 Kaskazini mwa mji wa Bukoba, hadi watakapomaliza ukarabati. Hadi hii leo ukarabati huo haujakamilika. Haijulikani itakuwa lini... Bila shaka linahitaji maombi ya sala na misaada.

Waliopita hapa Mpooo?


Du! Mzee Sumo Aponea Tundu la Sindano


Mzee wa Sumo kapata ajali mbaya huko Lindi, lakini ametoka mzima buheri wa afya. HAPA kaandika mwenyewe kuwa "Jamani wapendwa sijakuwepo kwa muda kwani nilisafiri kwenda Ntwara na jana ndio hii kitu ilinikumba baada ya kubiringika mara kadhaa!!!! Kikubwa ni kwamba bado nipo sijafa. navinjari Lindi ndio nikasema niwasalimu. lakini mchuma tuliokuwa tunasafiria ndio kwisha kazi!

Monday, April 27, 2009

Picha ya Wiki


Picha hii ya Emmanuel Herman, iliibua mazwali mengi. Maelezo yake gazetini yalikuwa hivi: 'Askari wa Usalama Barabarani akimalizia mazungumzo na dereva wa daladala'

Abdul Atwaa 10m/- Maisha Plus


Na Zaina Malongo

MSHIRIKI kutoka Zanzibar Abdul juzi ameibuka mshindi katika shindano la maisha plus na kujinyakulia kitita cha fedha taslim shilingi millioni 10, baada ya kuishi kijiji kwa takribani siku 56.

Kwa matokea yaliyotolewa na watazamaji kupitia ujumbe mfupi uliokuwa ukitumwa na wananchi kupitia mtandaoni na televisioni ya taifa (TBC 1)

Mshindi huyo kutoka Zanzibar, Abdul ambaye alikuwa akishindana vikali na Mwanadada Upendo kutoka mkoani Mwanza ambae alijiwekea uwezo mkubwa sana lakini hadi kufikia mwisho wa mashindano mshiriki huyo hakuweza kuamini ukweli wa matokeo waliyoyatangaza majaji.

Katika ya mchezo huo ambao mshiriki kutoka Mwanza Upendo alikuwa hakionekana kuwa mshindi baada ya kuwa na pointi nyingi ambazo ziliweza hata kumshinda Abdul kwa kuwa na pointi nyingi hadikufikia wiki mbili za mwisho.

Wakati mshindi wa shindano hilo akikabidhiwa kitita cha sh mil 10 na baadae wote waliweza kupatiwa siku moja ya kukutana na kubadilishana mawazo katika mbuga za wanyama zilizopo Mikumi mjini Morogoro.

Kufuatia siku hiyo ya kutembelea mbuza za wanyama washiriki ambao watakaokuwa walengwa na wale wote ambao wamefanikiwa kuingia katika kinyanganyiro cha kumi bora.

Washiriki hao ambao wameingia kumi bora na baadae kubaki washiriki watatu na ndipo alipochaguliwa mshindi mmoja na kujinyakulia shilingi milioni kumi ambayo ataweza kuwekewa kwenye akaunti yake kwa ajili ya usalama zaidi.

Washiriki hao ambao waliingia kumi bora ni Abduli,Modersta,Steve,Hamis,Maulid.



Tanzia

Mazungumzo ya mwisho na Mzee Phares Kabuye

Na Reginald Miruko

Juzi nilitoka Biharamulo, mkoani Kagera, kwenye mapumziko yangu. Siku naelekea huko, kwenye basi la Nyehunge mjini Mwanza, nilimuona Mzee Phares Kabuye.

Huyu ni mbunge wa zamani wa Biharamulo Magharibi, aliyewahi kuongoza jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo katika miaka ya 90 na baadaye kuondolewa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwa amemaliza miezi 20 ya kipindi cha tatu.

Kama mwandishi wa habari, wazo lilinijia kwamba nikifika jimboni kwake, nifanye naye mazungumzo juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo ya jimbo, rufaa yake katika Mahakama ya Rufaa ambayo haisikiki kwa muda mrefu, hali ya kisiasa wilayani kwake na mambo mengine. Hilo halikuwa taabu, kwani tulikuwa kwenye safari moja ya saa kama sita hadi mjini Biharamulo.

Tulipofika Sengerema na basi kusimama, nilipata wasaa wa kuwasiliana naye, na kuomba miadi ya mazungumzo. Kama ilivyo kawaida yake, hakushanga, alikubali. Akanipa namba yake ya simu na mimi nikampa yangu, tukakubaliana kukutana baada ya Sikukuu ya Pasaka.

Siku mbili baada ya Pasaka, nilimpigia simu nikamkumbusha miadi yetu, na kuomba kuonana naye siku hiyo. Alikubali moja kwa moja, akanielekeza kwake.

“Njoo, niko nyumbani kwangu, ni karibu na mnara wa Celtel (Zein),” alisema kwa sauti yake ya juu, iliyokuwa imezoeleka kulitikisa Bunge. Nilitafuta usafiri wa pikipiki ambao ni rahisi na unaopatikana kwa wakati wote mjini Biharamulo. Haikunichukua dakika tano kutoka eneo la Umoja nilipokuwa, hadi nyumbani kwake.

Kinyume na matarajio yangu, ghafla niliona kijana aliyenipeleka anasimamisha pikipiki. Akasema ni hapa tumeshafika. Nikamuuliza, nyumba ipi? Kijana huyo akajibu hii hapa. Nilijitahidi nisishangae sana, niliteremka, nikamlipa Sh500 za usafiri na kuelekea kwenye nyumba niliyoelekezwa.

Mbele ya nyumba hiyo walikuwapo wanawake wawili waliokuwa wakiaanika mahindi. Niliwauliza kama mzee Kabuye nimemkuta. “Yule palee, anayefukuza mbuzi,” alisema mwanamke mmojawapo.

Nilimfuata alipokuwa, nyumba kama ya tatu, tukarejea wote hadi ndani kwake. Tulikaa kwenye makochi na kabla ya kuanza mazungumzo, kama kawaida ya mwandishi yeyote nilitupa jicho hapa na pale sebuleni kwale.

Niliona magunia kadhaa ya mahindi ambayo baadaye alikuja kukiri kuwa ni mazao yake ya kilimo, kazi ambayo hadi kifo chake alikuwa akiifanya. Ukutani kulikuwa na picha kadhaa, mojawapo amepiga na Waziri wa Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo John Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Biharamulo Masharikii na nyingine akiwa anasalimiana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Katika mazungumzoa yetu, Mzee Kabuye alisema matumaini yake ameyaweka kwenye Mahakama ya Rufani, akiamini kuwa kama watenda haki, atapata haki yake na kuepuka kulipa mamilioni ya fedha za fidia endapo atakubaliana na maamuzi ya Mahakama Kuu iliyotengua ubunge wake.
“Hayo mamilioni ya kulipa mimi sina. Nitakachofanya ni kusubiri kesi ifike mwisho, ninaamini nitapata haki yangu,” alisema Kabuye aliyekuwa na umri wa miaka 71.

Alisema endapo kesi yake itafikia mwisho na nafasi ya ubunge kutangazwa au ikichelewa hadi uchaguzi mkuu mwakani, atagombea tena nafasi hiyo.

Hakuona kama umri wake umekwenda? Akijibu swali hilo, alisema: “Ubunge ni wa wananchi. Ikifika uchaguzi watu wengi wanajitokeza, wamo vijana, wako wazee, wako wanawake, wananchi wanachagua wanayemtaka. Tukibaguana huyu mzee, kesho tutasema huyu mwanamke, kesho huyu kabila sio kabila letu. Huko bungeni hatuendi kukimbia wala kupigana ngumi, ni hekima na busara.

“Wananchi wanakwambia shida zao na nyingine unaziona mwenyewe, unazipeleka bungeni. Basi. Na Wananchi wa Biharamulo hawachagui chama wanachagua mtu,” alisisitiza Kabuye ambaye pia alikuwa mbunge wa Bunge la Afrika.

Akizungumzia matatizo ya wananchi wake, alisema ni mawasiliano ya barabara zinazounganisha wilaya hiyo na maeneo mengine na umaskini. Barabara nyingi zenye matatizo ni za mkoa na taifa.

Alizungumzia barabara ya Kagoma-Lusahunga ambayo mkandarasi alisimamishwa na serikali, lakini haijatangaza hatua dhidi ya waliOmpatia zabuni wakati hana uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Yeye binafsi anapambanaje na maisha baada ya kutenguliwa kwa ubunge wake? “ Kwa sasa mimi ni mkulima. Ninalima mahindi na pia nina shamba la migomba. Hivyo ndivyo vyanzo vyangu vya mapato kulipa madeni na hasa mkopo wa bunge. Kuna miezi inapita bila kulipa.”
“Nilipovuliwa ubunge, hata kwenye Bunge la Afrika sikwenda tena. Kwa dhamira safi niliacha kwenda. Ukiendelea huo ni ufisadi kama ufisadi mwingine, maana ubunge huo wa Afrika niliupata kupitia bungeni.

Kuhusu hali ya kisiasa wilayani Biharamulo na kwenye chama chake cha siasa, mzee huyo alisema: “Huo mgawanyiko unaosikia huko juu hapa haupo. Sisi tunashirikiana kama kawaida. Tuna ushirikiano wetu na mwenyekiti wetu wa wilaya ni Martini Raphael wa Chadema.

Mzee huyo ambaye alieleza nia yake ya kuhudhuria mkutano Mkuu wa Tanzania Labour Party (TLP) unaotarajiwa kufanyika kesho, alidokeza nia yake ya kuwania tena nafasi ya Umakamu Mwenyekiti (Bara) na ujumbe wa Halmashauri Kuu (seneti) alizokuwa anashikilia kabla ya kifo chake.

Hata hivyo alikuwa makini kuzungumzia mgogoro kati ya Mwenyekiti wa TLP anayemaliza muda wake Augustino Mrema na baadhi ya wanachama wake kuhusu uchaguzi wa kesho:
“Chama si mtu; Mrema anaweza kutofautiana na baadhi ya wanachama au wanachama wakatofautiana na chama kikaendelea. Migogoro ya sasa siwezi ‘kucomment, sikuwapo, sijui sababu ya ugomvi wao, sijaongea na Mtungirehi wala Mrema,” alisema.

Baada ya mazungumzoa hayo tuliagana na nami nikaondoka, nikitarajia kuchapisha mahojiano nifikapo Dar es Salaam baada ya mapumziko yangu. Baada ya siku tatu, nikiwa mjini Bukoba, Mzee huyo alinipigia simu tena akitaka nirejee kwake, kwa sababu alikuwa na nyongeza ya mazungumzo.

Nilipanga naye miadi na tulipokutana, alinieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha serikali wilayani humo kuwataka wananchi wa kitongoji cha Isesa Maharage, kijiji cha Lusahunga wahame kupisha eneo la mgodi wanalodaiwa kuvamia.

“Mkuu wa wilaya amewataka wananchi wote wahame. Wengine wamekaa muda mrefu na wamefuata taratibu zote za kuishi hapo, mimi sioni sababu ya kuwahamisha wote, wangefanya uchunguzi na kubaini nani wa kuhama na nani ana haki ya kukaa hapo,” alisema.

Jana, baada ya kuripoti ofisini na kuanza kuandaa mnakala yake, nilipata taarifa za kifo chake, kutokana na ajali ya barabarani iliyomkuta akielekea jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo wa TLP. Bwana ametoa, bwana ametwaa, jina lake linarikiwe

Sunday, April 26, 2009

JK Ateua Mtuhumiwa wa Rushwa

Rais Jakaya Kikwete ameteua mtuhumiwa wa rushwa, Anatory Choya (pichani), mwenye kesi katika Mahakama ya Wilaya Biharamulo kuwa DC wa Kishapu, kabla ya kumuapisha kuanza kazi, akashtukia 'kashfa' hiyo, akamtemesha kimya kimya akiwa njiani na familia yake kwenda kuapishwa; hapo hapo akamteua mwingine kuziba nafasi yake Habari Kamili

Saturday, April 25, 2009

Samaki Adimu Wapatikana

Samaki huyu (namfahamu kwa jina la mbojo) aliadimika mno katika ziwa Victoria baada ya uujio wa Sangara, lakini hivi sasa ameanza kupatikana kwa wingi kwa sababu ambazo bado nazitafuta. Picha ya chini mchuuzi wa samaki hao akielezea utamu wake unaozidi samaki wengine wanaopatikana kwenye ziwa hilo


Utambulisho wa Bukoba

Kagera panajieleza. Picha ya juu ni pilikapilika za sokoni Bukoba mjini na chini ni shamba jipya la migomba, katika eneo la Kyagati, Kitongoji cha Buhesi, Kijiji cha Irogelo, Tarafa ya Kamachumu


Friday, April 24, 2009

Mto Ngono Wafurika!

Mto Ngono ukiwa unakaribia karibu na kingo za daraja la Kyabakoba wilayano Muleba, huku katikia picha ya chini maji ya mto huo yakipita juu ya barabara hatuia chache kabla ya daraja hilo. Hali hii ni hatari, huenda ikawarejesha wakati wa Kamachumu kwenye shida waliyoisahau kwa muda mrefu


Mzee Kabuye Is No More

Mzee Phares Kabuye, aliyekuwa mbunge wa Biharamulo Magharibi akiwa mbele ya nyumba yake mjini Biharamulo, Kagera tulipofanya mazungumzo naye wiki iliyopita. Leo amefariki katika ajali ya basi wakati anaelekea Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu wa TLP. Katika Mkutano huo alisema angewania tena nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Bara) na ujumbe wa Halmashauri Kuu (seneti). Nimeandika Obituary (tanzia) kwenye gazeti la Mwananchi. Isome hapa

Naangaza Upya kutoka Kijijini

Nawasalimu sana wanablogu walionivumilia kwa wiki kadhaa wakati sipatikani hewani. Mawasiliano haya yalikuwa 'mashokolomageni' huko nilikokuwa. Picha hii inajieleza yenyewe. Karibu tuendelee.

Thursday, April 09, 2009

Kumbe DECI ni Maelfu!




Maelfu ya wanachama wa DECI wakifuatilia hatma ya shirika lao la 'kupanda pesa na kuvuna pesa. Wenyewe wana matarajio makubwa kuliko kupoteza fedha zao kama wanavyosema hapa

Tuesday, April 07, 2009

Waziri Azungumzia DECI

Wakati vumbi la mchezo wa 'kupanda na kuvuna pesa' halijatulia, mshiriki mmoja wa mjadala mtandaoni kamuuliza Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, atoe commnets kwenye mchezo huo.
Mhe. Mahanga, tumejadili sana hapa suala la ubunifu, na namna ya kuwatoa vijana, je hii (DECI) haiwezi kuwa fursa muhimu zaidi? Maana miongoni mwa matatizo yanayodidimiza ubunifu na uthubutu miongoni mwa vijana ni kukosa mitaji, kama DECI wanasaidia kupata mitaji, kwanini wasisaidiwe? Kama kuna vita ya mapapa napo tuambiwe jamani, maana BONGO hatuchelewi!
Ahsante
Lingson


Baada ya swali hilo Waziri Mahanga alimjibu yafuatayo:
Lingson,
Baada ya ufafanuzi mzuri wa CMSA na BOT, hili la DECI mimi sikutaka kulijadili tena, mpaka uliponitaja kwa jina. Na nilikuwa na sababu mbili: Kwanza mimi siamini katika uwezeshaji wa watu (wakiwemo vijana) kwa njia ambayo siyo endelevu, kwa scheme ambayo ni wazi ni ya kibahati nasibu! Wanaoanza mwanzo wanapata, na wale wa mwisho watakosa! Kama waziri anayetakiwa kuwashauri vijana kuwekeza vizuri siwezi kuwaambia watumie fedha zao kucheza bahati nasibu. Bahati nasibu huchezwa na mtu kwa hiari yake kwani kuna kupata na kukosa, na unapata kwa sababu wengine watakosa! Hivyo ndivyo ilivyo DECI na schemes kama hizo. LAZIMA WENGINE WENGI WATAKOSA - PALE MPANGO HUO UTAKAPOANGUKA, NA HAKIKA KAMA KILIVYO KIFO CHA BINADAMU, MPANGO HUO NI LAZIMA UFE LEO AU KESHO!Lakini pili, sikutaka kujadili sana kwa sababu ya fani yangu na utaalamu wangu wa masuala ya fedha. Basically mimi ni mtaalamu wa fedha, baada ya kupata shahada ya juu kabisa kwenye uhasibu (CPA) baadaye digrii yangu ya pili ilikuwa kwenye masuala ya fedha (MSc. Finance). Najua kwa uhakika kwamba, ukiacha uwekezaji wa speculation, ROI (return on investment) kwa uwekezezaji wa kawaida, kama huu wa wanachama wa DECI haiwezi kamwe kuwa asilimia 300 - I mean, kwa wawekezaji wote. Kama wengine wamepata faida ya asilimia 300, hakika wengine watapata hasara ya asilimia 300! Hawa nitawajibu nini kama mimi ndo niliwashauri kuwekeza huko?Hapana Lingson, vijana siwezi kuwashauri kuwekeza huko DECI and the like.
Milton
Nyongeza ya Gazeti la The Citizen: Revealed: Deci has no account na nyingine iliyoandikwa juzi kuwa mchezo huo ni wa pyramid, ambao kwa vyovyote vile, utamalizika kwa watu kuliwa kwa kuwa wengi wanawachangia wachache, hivyo serikali inataka kuingilia 'kuwalinda' watu wake. Isome. Authorities prepare to act against Deci

Tangazo la DECI

Nimesikia tangazo Wapo Radio kutoka kwa uongozi wa DECI kuwa, leo Ofisi zote zimefungwa 'kuadhimisha kumbukumbu ya Karume'; Kesho pia zitafungwa kutoa nafasi kwa wanachama 'wanaopanda na kuvuna fedha' kujumuika katika mkutano wa wanachama wote katika ukumbi wa PTA, Sabasaba. Wasiwasi wangu, wenye mradi watajitokeza hadharani hiyo kesho, au ndo hivyo tena! Lakini, Cheki Hapa wenye mioyo migumu waliendelea kupanda na kuvuna hiyo jana.
Karume Day Njema!

-RSM-

Concluding Press Conference Video

Kwa Video hii, ndivyo mkutano Shirika la Makazi ulivyofungwa huko Nairobi

Sunday, April 05, 2009

Sababu ya Kupotea


Nilikuwa nimesuasua kidogo. Job ilizidi katika Mkutano wa 22 wa Barza Kuu la Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa-UN-Habitat-GC 22. Mkutano huo ulihudhuriwa wajumbe 797 kutoka katika nchi 104, kati yao wajumbe 500 wakiwakilisha serikali za nchi zao. Waliungana na watu 175 wanaowakilisha Mashirika yasiyo ya kiserikali, 41 kutoka serikali za mitaa na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali duniani. Picha zaidi cheki kwenye Album yangu hapo kulia.

Swali la Kuokota

Kuokota si kuiba: Swali hili nimeliokota kwenye Bidii@googlegroups.com

Ndugu Zangu,

Nimekuwa najiuliza ni kwa nini waandishi wa habari wa Tanzania ni rahisi sana kuwa “twisted’ kiasi ambacho wako tayari kutetea uovu kwa nguvu zao zote?. Je ni kwa kuwa biashara yao ni ngumu sana kiasi ambacho bila kununuliwa hawata”survive” au ni kwa kuwa taaluma ya Uandishi wa Habari haina “Professional Ethics” zinazoongoza taaluma hiyo?

Je mishahara ya waandishi wa habari ni midogo sana kama ya Polisi wa Usalama barabarani? Singeshaa sana kama wanaotetea uovu huo wangekuwa waandishi wachanga ambao wamesomea kwenye hivi vyuo “disposable”. Cha ajabu ni kwamba wakongwe ndo wamejiingiza kwenye kutetea maovu. Mfano mzuri ni hili suala la Dowans na binamu yake Richmond. Walioko mstari wa mbele kuwatetea waovu hawa waliovuna pesa zetu bila kupanda ni Waandishi wa Habari tena wakongwe!

Je inawezekana kuwa baada ya umri kupitiliza bila wakongwe hawa kuwa na “defined future” wameona bora watoke kupitia Dowans?

Nawakilisha.

Thursday, April 02, 2009

Hapo Mjini Naii


Hapa nikiwa kwenye ofisi za UN mjini Nairibi kwenye mkutano wa 22 wa Baraza Kuu la UN-Habibat.

Wednesday, April 01, 2009

Mchongo Kwa Journalists

Online Course in Science Journalism (FREE)

An online course in science journalism that covers major practical and conceptual issues in science journalism has been launched in English, French and Arabic by the World Federation of Science Journalists in close cooperation with SciDev.Net, the London-based Science and Development Network

The course was designed for use by professional journalists, journalism students and teachers. It consists of eight lessons on topics including: how to find and research stories, exposing false claims, how to pitch to an editor, turning crisis reporting to advantage and more.

Each lesson consists of an e-lecture with examples, self-teaching questions, and assignments.

To learn more and to get started, go to http://www.wfsj.org/course/


SOURCE: CLICK HERE
MAKULILO Jr, www.makulilo.blogspot.com

JK na miaka 20 ya ndoa



Rais Jakaya Kikwete jana alitimiza miaka 20 ya ndoa yake na Salma.
Sherehe hizo za kuadhimisha miaka hiyo 20 ilifanyika Ikulu jana jioni
ambapo keki ilikatwa na wawili hao walilishana keki hiyo kwa bashahi
mbele ya familia na jamaa ya karibu.
Pichani wakikata keki pamoja na ya pili mzee akimlisha mama keki.
Lukwangule inawatakia kila la heri katika familia hii ya kwanza ili
kuweza kuiongoza vyema familia yao na nchi.

chanzo; lukwangule entertainment