Saturday, February 26, 2005

Enyi Wanasiasa nani aliyewaroga?

Usipotafakari sana, utadhani wanasiasa wetu wamerogwa. Labda ndivyo falsafa za siasa zinavyotaka. Katika nchi yetu sasa wanasiasa tayari wameanza mambo yao ya kujikomba kwa wananchi kana kwamba hawajawahi kuwakosea.
Utashangaa sana kumwona mbunge akiwa jimboni akisimamisha gari kumsalimia kila anayekutana naye. Shikamoo zinatolewa hata kwa watoto! Ala, kumbe mpiga kura ni mfalme! Kama ni mfalme mbona ulimpuuza miaka yote ulipokuwa unalamba asali peke yako mjini Dodoma?
Wengine wameanza kulalamika hadharani kuwa majimbo yao wameingiliwa na wagombea wengine, wanaotaka kuyapora kana kwamba majimbo hayo ni urithi wao. Ebo, sasa mnacheza mchezo gani huo? Bravo Philip mwana wa Mangula kwa kulikemea hilo, na kuweka bayana kuwa, Jimbo ni Mali ya Wananchi.
Ole wao wale waliotamka wazi mbele ya wapiga kura wao kuwa wasitegemee msaada wowote kutoka kwa mbunge kwa kuwa kura walizompa zilibadilishwa sawa kwa sawa na pesa alizowalipa wakati wa uchaguzi (kula). Sorry, nazungumzia takrima. Je kauli hiyo inaweza kutoka tena? Labda kama mhusika amevuna takrima kubwa zaidi katika ubunge wake.
Kutokana na hayo, naona kuwa baadhi ya wanasiasa wamerogwa kama walivyorogwa Wagalatia kwenye misaafu. ndio maana nauliza hivi:
Enyi wanasiasa nani aliyewaroga?. Angalizo: takrima ni rushwa isiyokubalika kabisa ndani ya chujio la CCM la wagombea, lakini ni ruksa katika uchaguzi unaoshirikisha vyama vyote vya siasa.

Njia ya Ikulu ni nyembamba kama ya Mbinguni

Mbona wanangu mnakanyagana wakati njia ni pana sana? au mnadhani njia hiyo ni nyembamba kama ya mbinguni?
Maswali hayo ndiyo unayoweza kuwauliza wazee wetu wakati huu, hasa ukishuhudia pilikapilika zao za kutaka kwenda Ikulu. wanashikana mashati si utani, Wanariadha wetu katika mbio hizo za Ikulu, wasiojali kuogopwa kama Ukoma (rejea hotuba ya mwalimu Nyerere kwa wanaokimbilia ikulu, 1995), wako katika kasi ya ajabu.
Wengine wanatembelea wajumbe wa NEC, Mkutano Mkuu wa CCM na 'kuwawezesha', wengine wamenunua magazeti na vyombo vingine vya habari. Juzi, mjini Dodoma, gazeti moja jipya la kila wiki, lilichapisha habari katika uk. wa kwanza kuwa, Baraza la Mawaziri la mmoja wa wagombea urais limevuja. Waliomo wakatajwa waziwazi. Tulishangaa, Nakala za gazeti hilo zilikusanywa mtaani kwa gharama zozote ziwazo na kuteketezwa na ama wapambe au mgombea mwenyewe.
yangu macho, natarajia vituko zaidi na ninazidi kuwaona wakichafuana. Mie, Kama Mkapa. Sina Mgombea.

Wednesday, February 23, 2005

Kipenga kimelia....On your marks, gets ready. Go....

Machi Mosi iko mlangoni. Ni tarehe muhimu kwa wapigania ulaji ndani ya Chama Twawala, CCM. Ndiyo siku iliyopangwa kuanza kuchukua fomu za kuingia jumba 'takatifu', ingawa sina uhakika kama wanaolikalia wote ni watakatifu kama lenyewe.
washiriki wa mbio hizo ni wengi, baadhi wamejitaja na wengine badi ingawa dalili zinaonyesha kwamba watajiunga katika mbio hizo za kupokezana vijiti.
Wakati wakimbiaji wanajitokeza kwa wingi, muda nao haujatulia. Unakwenda mbio. Huwezi kuamini, miaka 0 tayari imekwisha na Mzee Mkapa kamaliza muda wake wa kukaa Ikulu, kuzungukwa na walinzi na zaidi ya yote kukosa uhuru binafsi, japokuwa ana mamlaka makubwa, 'yanayokaribia' kuwa juu ya sheria. ka kweli, mzee huyu kaacha mambo mengi mazuri sebuleni na rekodi chache mbaya chumbani ikiwemo ya mauaji ya Wapemba wa Civic Unitred Front (CUF) ya Januari 26 na 27, 2001.hatujui atamwachia namni kazi hiyo ya juu kabisa nchini. Je, ni wale waliojitangaza, kina Sumaye, Simba au wanapotajwa kina Kikwete, Malecela, Mwandosya na....Yetu macho....

Saturday, February 12, 2005

Wakubwa wameondoka, Dodoma imenuna tena

Jana, Ijumaa Mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Muungano uliahirishwa. Mheshimiwa sana Spika Msekwa alitoa ruksa kwa Waziri Mkuu Sumaye kuahirisha bunge hadi April. Kuanzia leo, wakubwa wameanza kurejea kwenye mji wao wa joto, Dar. Ingawa misaafa ya hapa kwetu inasema Dodoma ndio mji mkuu wa Tanzania, ukweli ubaki pale pale kuwa makao makuu halisi yapo Dar es Salaam, mji wenye vivutio vya kila aina. Ndio hivyo tena wazee wameondoka. Mashangingi (Landcruiser) nayo yamepungua mjini. Vimebaki vigari gari vilivyochakaachakaa. hakutatokea magari ya gharama kubwa kama hayo kugongana tena kama ilivyokea majuzi, ambapo gari la Waziri Migiro na Mbunge Kasaka yalipobamizana uso kwa uso.
Katika Bunge hili kuma mambo mengi yaliyoleta changamoto, moja kuwa lilikuwa la mabadiliko ya katika ya nchi, ambayo hata hivyo, Kambi ya Upinzani imesema yalikuwa danganya toto. Imepita kwa kura za wabunge wa CCM pekee baada yawake wa upinzani ku-'walk out', isipokuwa wale wabunge wawili wanaobezwa na wenzao kuwa ni mahakama. (walifukuzwa na vyama vyao, mahakama ikawarejesha. Kutokana na uamuzi huo, Sumaye amewabeza kuwa hawajui kanuni za bunge, wamekimbia mjadala badala ya kukaa na kujenga hoja.
Kubwa zaidi, mbali na shughuli za bunge, vyombo vya habari vilitawaliwa na issue ya kukombea urais wa Tanzania. Wiki ijayo, Halmashauri Kuu wa CCM inakutana hapa kupitisha pamoja na mambo mengine, ratiba ya uchukuaji fomu za kuomba kugombea urais kupitia chama hicho hapo Machi. Hapo ndo tutaona kivumbi na jasho, mbio kali kali na chafu, ilimradi kila mtu aingie IKULU ya Chamwino, sorry, ya Mtaa wa Lutuhuli, Dar es Salaam.

Friday, February 04, 2005

UTABIRI UMETIMIA:'Makao Makuu yako Dodoma'

YALIYOTABIRWA yameshatimia. Makao Makuu ya nchi sasa yako Dodoma. Waheshimiwa wote, isipokuwa rais na amakamu wake, wamejaa hapa tele kama pishi la mchele. Ukitembea mji mzima wa Dodoma, unakutana tu na magari ya kifahari, ambayo hayapo popote Afrika. Haya ni 'mashangingi' au kwa jina lake halisi Toyota Landcruiser ama GX au VX. Ukiingia baa utakutana na waheshimiwa wale wale.
Kilichowakalisha hapa pamoja na mambo mengine ni kupitisha Mabadiliko ya 14 ya Katiba. Yaani tangi nchi ipate katiba yake ya sasa mwaka 1977, imeshawekwa viraka 14 na wabunge wanasema hoja na maoni yote ya wananchi, waliyojadiliwa na kupitishwa katika waraka namba 1 wa serikali 'white paper' juu ya katiba hayakuzingatiwa yote. Hapa ina maana kwamba katiba yetu itaongezwa viraka vingine zaidi, na unaweza kuikuta katika hali ambayo haijulikani kitambaa kilichotangulia kilikuwa na rangi gani! si maajabu hayo!
Hoja za baadhi ya wabunge achilia mbali wale 'mbumbumbu wa sheria, ni za msingi, lakini hazimo katika katiba ya sasa; na wale wachache 'wenye nchi' hawafikirii hata kidogo kuyaingiza. Tunaendelea kuwa na 'waheshimiwa' hawa hapa Dodoma hadi mwisho wa wiki ijayo.
Tutaelezana yanayojiri.