Thursday, August 10, 2006

Ukasuku si Kipimo cha Uzalendo

Mjadala wa Filamu ya Darwin's Nightmare iliyoandaliwa na Hubert Sauper raia wa Australia anayeishi Ufaransa umepamba moto. Baadhi ya watu na taasisi wamejikuta katika ya mjadala wenyewe. Gazeti la Mwananchi lilichapicha maoni (editorial) haya Agosti 8, mwaka huu ili kujibu baadhi ya mambo.

Dar es Salaam, Agosti 8 2006


Ukasuku si kipimo cha uzalendo

BAADA ya hotuba ya mwishoni mwa mwezi uliopita ya Rais Jakaya Kikwete, ambayo pamoja na mambo mengine alizungumzia suala la filamu ya ‘Darwin’s Nightmare' kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imejikuta ikishambuliwa na baadhi ya watu bila sababu zozote za msingi.

Mashambulizi haya yametolewa na waandamanaji walioamua kumuunga Rais mkono huko mkoani Mwanza kutokana na hotuba yake ambayo ilibeza maudhui ya filamu hiyo ambayo inadaiwa kwamba yalilenga kuidhalilisha Tanzania na hususani wakazi wa mkoa huo.

Wakiwa wamebeba mabango yaliyowashutumu wote waliohusika katika utayarishaji wa filamu hiyo, na baadhi yakielekezwa kwa kampuni ya MCL hususan gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, waandamanaji hao walionyesha wazi kwamba hawakufurahishwa na filamu hiyo na hivyo kukubaliana na kauli ya Rais kwamba ililenga kuwadhalilisha.

Si nia ya tahariri hii kurejea mabango yote yaliyobebwa, lakini kwa manufaa ya wasomaji wetu tutataja moja wapo lililosema hivi: “Aga Khan gazeti lako The Citizen linatuharibia nchi yetu.”

Bango hili pamoja na mengine matatu yaliyochapishwa kwenye gazeti la Mzalendo la Jumapili Agosti 6, mwaka huu, kwa aina ya maandishi, wino uliotumika na uumbaji wa herufi yanaonekana kuwa ni kazi ya mtu mmoja. Kwa maana hiyo si mabango ambayo yanaonyesha hisia za watu mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza kwa sababu kwa kawaida watu wanaoshiriki maandamano kila mmoja huibuka na la kwake.

Kwa maana hii mabango hayo ni dhahiri ni kazi iliyopangwa kwa ustadi na mtu au kundi fulani la watu ili kuchafua si tu jina la The Citizen, bali hata mmoja wa wanahisa wa kampuni ya MCL. Hili halitushangazi na hasa ikizingatiwa kwamba watu wa kwanza kushabikia ni wa gazeti la Mzalendo ambao bila haya walitoka na kichwa cha habari kikiongoza ukurasa wa mbele kikisema: “Mwanza wasema gazeti la Citizen halina nia njema.”

Tunapenda kuweka sawa mambo kadhaa katika suala hili lote. Moja kuna upotoshaji wa makusudi kabisa unaofanywa ili kuharibu sifa njema na iliyotukuka ya gazeti la The Citizen. Huu si uzalendo hata kidogo.

Lakini kikubwa ni lazima tusema hapa kwamba kwa ufahamu wetu hatuoni ni wapi The Citizen inaweza kubebeshwa lawama yoyote katika suala zima la filamu hii ya Darwin’s Nightmare. Tunasema haya kwa kuwa chimbuko la filamu hii ni kuonyesha jinsi uvunaji wa rasilimali za nchi hii usivyonufaisha wananchi wake.

Filamu hii imejikita kwenye dhana ile ile ya uvunaji wa rasilimali za nchi za ulimwengu wa tatu ambao unanufaisha mashirika ya kimataifa ya nchi zilizoendelea huku nyuma ukibaki umasikini wa kutupwa wa watu wake. Ndivyo ilivyo kwa nchi za Afrika zinazozalisha madini kama dhahabu, mafuta ya petroli mazao ya misitu na kila aina ya maliasili ambazo muumba alijalia nchi tofauti duniani.

Kwa maana hiyo, filamu hii si tu inaonyesha jinsi umasikini unavyoendelea kubakia katika jamii yetu licha ya kuzungukwa na utajiri mkubwa wa rasilimali ambazo zinavunwa na kuchukuliwa na wakubwa wa dunia hii, yaani wababe. Hii ndiyo hoja ya msingi iliyo mbele yetu.

Kinachotokea katika ziwa Victoria kuhusu biashara ya minofu ya samaki hakina tofauti yoyote na kinachotokea katika migodi mikubwa ya madini ya dhahabu na ndiyo maana serikali ya awamu ya nne imeamua kupitia upya mikataba ya uchimbaji madini ili nchi kama taifa ifaidi maliasili zake.

Juzi na jana tuliandika katika gazeti hili jinsi minofu ya samaki inavyouzwa kwa bei ya juu huko Ulaya. Wakati kilo mbili ya samaki wanaonunuliwa kwa wavuvi huweza kutoa mnofu wa kilo moja hununuliwa kwa wastani wa Sh2,000, mnofu huo ukifika sokoni Ulaya huuzwa kwa wastani wa Sh20,000 kwa kilo, kwa maneno mengine bei hiyo ni mara kumi zaidi ya bei anayouza mvuvi katika ziwa Victoria. Hata kama ikijumlishwa na gharama za uzalishaji na usafirishaji, bado anayeonekana kufaidi hapa kwa kiwango cha juu kabisa ni ni watu wa kati na makampuni yenye viwanda hivi.

Kwa hiyo, Darwin’s Nightmare si tu ilijikita kueleza jinsi umasikini unavyowaandama Watanzania waliozungukwa na ziwa hilo kubwa kuliko yote barani Afrika, bali pia inaonyesha nadharia ya mwenye manguvu ndiye anayefaidi. Hatuna uhakika kama wengi wa wale walioandamana wanalifahamu hilo.

Lakini kikubwa zaidi hakuna uwezekano wa kubadili ukweli kwamba wananchi wa Mwanza wanakula mapanki kwa sababu samaki aina ya sangara wameadimika mno kutokana na viwanda hivyo, pia maandamano haya hayawezi kuua ukweli kwamba makampuni haya ndiyo yanayonufaika zaidi kuliko taifa na watu wake kwa ujumla.

Tukiachia mbali hayo yote, mtayarishaji wa filamu hii, Hubert Sauper, hakuingia nchini kinyemela na kuanza kutayarisha filamu hiyo. Alifuata taratibu zote zinazokubalika ikiwa ni pamoja na kuwasilisha rasimu (script) ya alichokusudia kwenye vyombo husika. Alikubaliwa na alilipa ada zinazostahili.

Filamu hii ilitayarishwa mwaka 2003 na kuanza kuonekana huko Ulaya mwanzoni mwa mwaka 2004, wakati huo gazeti la The Citizen lilikuwa hata halijaanza kuchapishwa. Kwa hiyo kuliunganisha gazeti hili na filamu hii ni upotoshaji mkubwa, lakini kikubwa zaidi hata kama filamu hii ilikuwa na lolote la maana la kuripotiwa kama The Citizen ililiona na kuliandika kama gazeti limefanya kosa gani?

Juzi katika gazeti la Mwananchi Jumapili tulisema wapo watu wanaotaka kuingia katika ukasuku wa kutaka kufurahisha wengine. Tuna uhakika wapo waliofanya maandamano hayo bila kujua kwa yakini maudhui ya filamu hiyo. Hawa wametumiwa! Hawajaiona filamu na hata hawajui kilichomo ndani kina ukweli gani hata kama wao wenyewe umasikini unawahemea shingoni. Hawa ni watu wa kuhurumiwa.

Lakini kwa wale wanaotaka kutwaa madaraka ya kuwa wenye hati miliki ya kuzungumza katika nchi hii, kwamba wao ndio wazalendo kuliko wenzao, tungependa tu kuwakumbusha kwamba kila Mtanzania ana haki sawa na mwingine, wote sisi ni raia, hakuna wa daraja kwanza na wa daraja la chini, hakuna anayeweza kujiita mzalendo zaidi ya mwingine eti kwa sababu tu ya itikadi yake ya kisiasa. Hili tunalipinga na tutaendelea kulipinga. Hii ni nchi yetu sote.

Gazeti la The Citizen linaendeshwa na waandishi na wahariri Watanzania, tena wazawa. Wamesoma na kukomaa kwa elimu ya Kitanzania. Hakuna anayeweza kujitutumua na kuwabeza au kuwaona kwamba utaifa wao haujakamilika kwa sababu tu wanakataa kuwa kasuku wa kuimba kila kitu kisemwacho na wakubwa.

Tunapenda kusisitiza kwamba kulishupalia gazeti la The Citizen kwamba eti haliitakii nchi hii mema ni kulipaka matope na kulitaka liwe kasuku, kazi ambayo katu haliko tayari kuifanya. Tungependa kusisitiza kuwa maoni ya Watanzania wote ni sawa na kwamba kuwa mfuasi wa chama tawala hakumfanyi mhusika kuwa Mtanzania zaidi ya wengine.

11 comments:

Anonymous said...

RSM, nishasema kuwa taaluma ya uandishi inaenda kubaya, sasa mambo yanakuwa mazuri maana kuna baadhi ya magazeti yanaandika ukweli, tatizo letu ni la kuwa MISIFA kila wakati. SASA nataka kusema hao kasuku na wabunge wao wamepangwa kufanya hivyo na huo ujinga zaidi kuliko kitu kingine. Hii film ni ukweli halisi wa makuadi wa soko huria, na kama waheshimiwa wngekuwa na upeo basi nadhani hiyo ingetusaidia sana kuwakemea EU. Chaajabu wakati watu wanaandmana kuunga mkono kitu ambacho hawakielewi nchi za Ulaya sasa zinaanza kujadili kurekebisha mfumo huo wa ukandazaji wa kibiashara na pia kusisitiza zaidi FAIR TRADE, sasa wajinga wachache eti wanaandamana kupinga hali hiyo ili tuendelee kunyonywa, haiji kichwana nadhani unatakiwa kuwa na matatizo ndipo uelewe ama uandamane.
Si ajabu, mika fulani Mwalimu wakati eule alitoa hotuba pale KIGOMA lake Tanganyia studium, alisepinga mambo ya kushusha thamani ya shilingi yetu, akasema kwa ukali sana, nikiwa mwanafunzi chini ya mfumo wa chama kimoja tuliamuliwa kuandamana kuunga mkono hotuba hiyo. Msakini tulikuwa wajinga juu ya mfumo wa kiuchumi baada ya siku chache tukashusha thamani, hivyo maandamano yale ambayo kimsingi yalifanyika TZ nzima yalikuwa ni ya kiwehu sana, sasa na hao ambao wametengenezwa kufanya maandamano ili kuendeleza unyonyaji watasutwa na wajukuu zao. UKASUKU HATARI SANA NA KUPENDA SIFA NAKO KUNAPONZA MAANA SIFA ITATAWALA WALA UPEMBUZI HAUTOKUWEPO.Media TZ sionyeshe picha hiyo alafu tuone ni nani mkweli na ni nani anapotosha watu.Jmani tuna dhamana kubwa sana kuwahabarisha watu ukweli na kiongozo lazima awe mkweli na sio kupotosha, ningekuwa mimi ningezuia watu wasiandamane kuunga mkono uongo wangu.

mloyi said...

Kwani tatizo ni nini?
Kwani Kikwete hajajua kwamba kuna watu wanashauku ya kupata sangara na hawawapati?, Ingawa yeye amewaita 'masikini wachache' anatakiwa kutambua wajibu wake wa kutumia kodi za serikali kuhakikisha wanapata uwezo wa kujipatia samaki na milo yao kikamilifu.
Hakugusa neno soko huria kwenye hotuba yake, lakini tatizo ni soko huria, Miaka ya themanini niliishi Mwanza kidogo, kabla soko huria halijaingia kwenye sangara, sangara na minofu yake yote tulikuwa tunakula sisi wageniwa mwanza na wasukuma 'masikini'(kama wapo!) hakuna aliyefikiria hayo 'mapanki'. Wenyeji walikuwa wanakula Sato,Kamongo na tilapia. nashangaa ya leo.
Tujihadhari na hili soko huria.

Anonymous said...

Zama zile pale nje station ya Mwanza minofu ya samaki ilikuwa kibao.Sasa hivi hapa Mwanza ni harufu ya mapanki tu yakizolewa na kusambazwa maeneo ya Mkuyuni na kwenda mbele mpaka huko Nyakato na vijiji vingine. Mimi nakaa Mwanza, sikithubutu kushiriki maandamano yao maana ni ya kisiasa mno, ukweli unabaki paleplae hayo maandamano hayakubadili chochote kilichomo katika film ile. Alafu wakati wa maandamano ya aina hii umeshapitwa na wakati wa chama kimoja, JK asitake kutafuta sapoti baada ya kuchemsha, tuna mtazamo mkubwa na kwa upeo sio tu kutafuta ufahari, tutegemee kushuhudia ujinga mwingi siku za mbeleni.

Simon Kitururu said...

Mimi kinachonisikitisha zaidi ya hili swala la samaki ni ukweli kwamba eti Tanzania tunadhibitiwa kutumia maji ya ziwa hili hata wakati wa ukame kwa mkataba waliokubaliana Wamisri na Waingereza. Ndio labda ni kweli matumizi ya maji ya ziwa hili yanaweza kuathiri Mto Nile. Lakini je si ukweli pia Taifa inabidi lijali watu wake kwanza?Angalia nchi zote duniani ukianzia Marekani hujali wao kwanza. Sasa tumefikia hatua ya hata hao samaki kuwakosa .Sitashangaa likitokea jambo jingine la kiajabu ajabu linalotokana na ziwa hili

Anonymous said...

Binafsi nimeshangazwa na msimamo wa Rais wetu ambaye vinginevyo naamini ni kiongozi mwenye uwezo wa pekee kifikra na kimaono-alinitia moyo sana alipozungumza kuhusu madini-jambo ambalo mimi mwenyewe niliwahi kuliandikia katika jarida fulani la kitaaluma kwa mwelekeo huo huo. Mimi nilizaliwa Maeneo ya Ziwa Victoria-Mwanza, miaka ya mwanzo ya sitini. Naweza kukuhesabia kwa vidole aina kama tano au zaidi za samaki niliowaona na kuwala utotoni, ambao siku hizi nikienda Mwanza ni hadithi tu tunasimuliana na dada zangu na kaka na wadogo zangu. Miaka michache iliyopita Nimeshuhudia kinyesi katika mifereji ya maji ya mvua barabarani, si kwingine, bali katikati ya jiji la Mwanza, lililobatizwa na wakazi wake 'zizi la Mwanza', ambao pengine baadhi yao ni hao hao waandamanaji. Mji unaozungukwa na machimbo tele ya madini, unaostahili kuwa mandhari nzuri lakini umegeuka 'slum city'. Pengine wandamanaji walipewa pilau na kusombwa kwa malori ya serikali yaliyo badilishwa namba kuwa ya binafsi kwa muda, au hata ya wanaviwanda-nani ajuaye? Pengine wanaviwanda walilipia kitu kidogo, nani ajuaye? Lakini msiache kabisa kuandika. Tena hawa waandamanaji wangalichukua muda kidogo tu kutafakari, wangalichagua kuandamana juu ya jambo lingine kabisa-ule mrabaha uliopigiwa kelele siku nyingi tu na mama mbunge wa jimbo mojawapo mkoani mwangu, Mongela. Leo tunambiwa ulikuwapo siku nyingi lakini mbona wahusika waliunnyamazia kimya na hata 'kuupinga'. Hapo nitaelewa watu wakiandamana. Enyi waandishi, msiogope. Mwanafalsafa Sokorati (Socrates) alisema kuwa daima kuna kundi kubwa la jamii linafuata mkumbo. Ukianzisha azimio, wataandamana kuunga mkono. Ukilifuta, wataandamana pia kuunga mkono, na bado ukifuta ufutaji huo, wataandamana kwa mabango makubwa zaidi wakisifu hekima yako inyojinyambulisa na yenye uchambuzi wa juu wa mambo. Lakini hakika siku moja uwongo utajitenga na wananchi wataweza kufurahia matunda ya rasilmali zao-hata kama ni kwa kushirikiana na hawa wageni-ambao sina kinyongo nao, tatizo ni jinsi wanavyoabudiwa na watawala. Kuna kichekesho cha serikali zetu za kiafrika pia: Kama kuna shida ya rushwa na inafanyiwa kazi na wanahabari, vyombo vya dola huingilia mara na kutoa msimamo sahihi na mtu yeyote akisema neno anaambiwa 'hakuna mtu mwenye taarifa sahihi kuliko Rais', na kwa kiasi hii inaweza kuwa sawa na kweli. Lakini ikifikia kwenye rushwa inayotoa harufu toka vinywani mwa watawala utasikia 'tuleteni ushahidi na taarifa'. Mwe!

Rama Msangi said...

Nasubiri kwa hamu sana kumsikia kesho akiongea na Watanzania (sujui ataongea nao kupitia wazee wa wapi), nione kama atagusia jinsi alichokiongea kuhusu mapanki kimezua mjadala au laa

Rashid Mkwinda said...

Huu ni ubabaishaji wa walio nacho kudhani kwamba kila mtu anaisha kama waishivyo wao, hawajui kwamba kuna wengine kutembea peku kumegeuzwa kuwa ni jadi kutokana na hali ngumu ya kumiliki angalau talawanda mguuni.

Hawajui kuwa kuna baadhi yetu huamua kufunga saumu kutokana na kutomudu kumiliki tonge la siku moja seuze minofu ya sangara ambayo husafirishwa kwa wenye nazo huko majuu.

Hawajui kuwa kuna baadhi yetu hulala vibarazani kwa kukosa mahali pa kulala na asubuhi kukicha huzurura mitaani na kuomba omba kwa waliojaaliwa chochote.

Hawajui kuwa kuna baadhi yetu tumeshindwa kumiliki angalau baiskeli ilhali kuna wenzetu ambao ni wale tuliowapigia KULA wakitembelea magari ya milioni lukuki bila kukumbuka hali ya maskini wliowaacha majimboni mwao eti leo wanasema filamu hiyo imelidhalilisha Taifa hivi hawa watu vipi.

Ni mapema mno kwani hivi viatu walivyovaa ikifika miaka mitano ijayo watasema kuwa haviwatoshi, mie wananiudhi sana hawa majamaa, wamekaa huko wanavimbisha vitumbo vyao na kulala usingizi katika viti ambavyo vimetokana na kodi za wakulima wa kahawa, pamba,alizeti, tumbaku, mahindi na hata mapanki.

Acha tu yaani hapa nimevimba sura kwa hasira kama anatokezxa mmoja kati ya hawa wanaodai kwamba hakuna watu wanaokula samaki waliooza naweza kumpiga NDOO ya kifuani yaani KUM'ZIDANE'

Anonymous said...

Mkwinda umekuwa Materrazi?

Anonymous said...

Maoni yako ni sahihi nashangaa kwa msimo wa serikali na hao wanaondamana bila hata ya kuitizama filamu yenyewe kweli huu ni ukasuku.Mimi nichukulia filamu hiyo kama kio kinacho onyesha hali halisi ilivyo lakini hao makasu ambao ninaima wengi waohata hiyo filamu hajaiona wanajaribu kupotosha ukweli.Msaswala makuu matatu ambayo naimani filamu inayaonesha 1.UMASIKINI KATIKA MAZINGILRA AMBAPO TUNALASILIMALI ZA KUTOSHA AMBAPO ZINANUFAISHA WACHACHE,2.RUSHWA KAMA RUSHWA IMETAWALA AMBAPO MWENYEPESA ANAWEZA KUFANYA LOLOTE ATAKALO AMBAPO KWAKUTUMIA RUSHWA MATAJIRI HAO WANAINGIZA SIRAHA KWANI SIRAHA NI BIHASHARA NZURI.3.UMALAYA MTENGENEZA WA FILAMU HAKUWA NA MAANA YA KUA UMALAYA UMEKITHIRI TANZANIA KWANI HAPA ULAYA UMALAYA NI KITU CHA KAWAIDA HAPA FILAMU ILITAKA KONYESHA NI JINSI GANI ILIVYO HATARI UMALAYA KATIKA MAZINGIRA YA UKIMWI.hAYO NILIYOYATAJA HAPO JUU SERIKALI HAIKUTAKA KUYAONA.KAMA MIMI NINGELIKUA RAIS NINGELIMPA MEDALI MTEGENEZAJI WA FILAMU HIYO KWANI NICHANGAMOTO KWA SERIKALI "DON’T BEAT AROUND THE BUSH"
Japhari Shabani St.Petersbug Russia

Ansbert Ngurumo said...

Nakubali. Tangu gazeti hili lianzishwe, halijawahi kuandika tahariri mahiri na makini kama hii. Naona sasa limetangaza rasmi kujinasua katika makucha ya watawala ambao wameamua 'kuyafuga' magazeti, redio na tv zote ili vyombo vya habari viimbe sifa zao. Viongozi wetu, badala ya kuchapa kazi, wameanza kampeni ya kuwania tena madaraka mwaka 2010. Aibu! Bahati mbaya ni kwamba wamedhamiria kuvitumia vyombo vya habari - hata visivyo vyao - kuwahadaa Watanzania. Ni vema Mwananchi nalo limeanza kutambua hilo na kukataa kufanya kazi chafu. Reginald, hebu nieleze, haya ni matokeo ya MAJUKUMU yako mapya? Hongera!

Ansbert Ngurumo said...

Naona huna majibu. Au umeyachelewesha tu?

Post a Comment