Saturday, February 26, 2005

Enyi Wanasiasa nani aliyewaroga?

Usipotafakari sana, utadhani wanasiasa wetu wamerogwa. Labda ndivyo falsafa za siasa zinavyotaka. Katika nchi yetu sasa wanasiasa tayari wameanza mambo yao ya kujikomba kwa wananchi kana kwamba hawajawahi kuwakosea.
Utashangaa sana kumwona mbunge akiwa jimboni akisimamisha gari kumsalimia kila anayekutana naye. Shikamoo zinatolewa hata kwa watoto! Ala, kumbe mpiga kura ni mfalme! Kama ni mfalme mbona ulimpuuza miaka yote ulipokuwa unalamba asali peke yako mjini Dodoma?
Wengine wameanza kulalamika hadharani kuwa majimbo yao wameingiliwa na wagombea wengine, wanaotaka kuyapora kana kwamba majimbo hayo ni urithi wao. Ebo, sasa mnacheza mchezo gani huo? Bravo Philip mwana wa Mangula kwa kulikemea hilo, na kuweka bayana kuwa, Jimbo ni Mali ya Wananchi.
Ole wao wale waliotamka wazi mbele ya wapiga kura wao kuwa wasitegemee msaada wowote kutoka kwa mbunge kwa kuwa kura walizompa zilibadilishwa sawa kwa sawa na pesa alizowalipa wakati wa uchaguzi (kula). Sorry, nazungumzia takrima. Je kauli hiyo inaweza kutoka tena? Labda kama mhusika amevuna takrima kubwa zaidi katika ubunge wake.
Kutokana na hayo, naona kuwa baadhi ya wanasiasa wamerogwa kama walivyorogwa Wagalatia kwenye misaafu. ndio maana nauliza hivi:
Enyi wanasiasa nani aliyewaroga?. Angalizo: takrima ni rushwa isiyokubalika kabisa ndani ya chujio la CCM la wagombea, lakini ni ruksa katika uchaguzi unaoshirikisha vyama vyote vya siasa.

No comments:

Post a Comment