Sunday, May 15, 2011

Chadema Shy wafafanua kuenguliwa Shibuda

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

HATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga kimetoa ufafanuzi kuhusiana na kutenguliwa kwa uteuzi wa Bw. John Shibuda kukaimu nafasi ya uenyekiti wa mkoa wa chama hicho.

Mara baada ya kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa CHADEMA mkoani Shinyanga, Bw. Philipo Shelembi, Baraza Kuu la uongozi la chama hicho katika mkoa huo lilimteua Bw. Shibuda kukaimu nafasi hiyo mpaka pale uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo utakapofanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Shinyanga, katibu wa CHADEMA mkoani Shinyanga, Bw. Nyangaki Shilungushela alisema uteuzi wa Bw. Shibuda ulitenguliwa na Kamati Kuu ya Taifa kwa nia nzuri ya misingi ya kuheshimu katiba ya chama.

Bw. Shilungushela alisema hatua ya kutenguliwa kwa uteuzi huo uliofanywa na baraza la uongozi la mkoa wa Shinyanga ilikuwa ni kwa nia nzuri na hapakuwepo na mizengwe ya aina yoyote wala nia ya kumkomoa Bw. Shibuda.

Alisema kamati kuu ilizingatia zaidi misingi ya katiba inayoelekeza pale inapotokea nafasi yoyote kuwa wazi kwa sababu zozote zile basi ni lazima ufanyike uchaguzi kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo na kwamba hakuna kifungu chochote ndani ya katiba kinachoelekeza suala la uteuzi wa kukaimu nafasi iliyowazi.

Alisema kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA mtu ambaye hivi sasa anapaswa kushika nafasi hiyo kwa muda, ni katibu wa mkoa hivyo yeye kama katibu ndiye anayekaimu nafasi hiyo badala ya Bw. Shibuda.

“Kutenguliwa kwa Bw. Shibuda hakuna sababu zozote za kimizengwe, bali ni utaratibu tu wa chama kwa misingi ya kuzingatia katiba yake, kwa hiyo kamati kuu imeliona hilo na sisi wana Shinyanga tumeafiki,”

“Lakini pia chama kimezingatia kwamba hivi karibuni patafanyika chaguzi katika mikoa mipya ya Katavi, Simiyu, Geita na Njombe ambayo inatarajiwa kuanza kazi rasmi mwaka wa fedha, hivyo pia na sisi wa Shinyanga tutafanya uchaguzi kuziba nafasi ya marehemu Shelembi,” alieleza Bw. Shilungushela.

Bw. Shibuda aliteuliwa na baraza la uongozi la mkoa wa Shinyanga kukaimu nafasi hiyo na yeye kuipokea kwa mikono miwili lakini hata hivyo uteuzi huo ulidumu kwa siku nne tu na kisha kutenguliwa na kamati kuu ya CHADEMA Taifa Aprili 30, mwaka huu.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment