Thursday, August 19, 2010

TAMKO LA VIONGOZI WA DINI KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA 2010

TAMKO LA VIONGOZI WA DINI KUHUSU UCHAGUZI MKUU WA 2010

Sisi Viongozi wa Dini kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar tuliokutana hapa Dodoma tarehe 18 Augusti 2010 kutafakari juu ya Hali ya Amani ya nchi yetu hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu.

TUNATAMBUA KWAMBA tarehe 31 Oktoba 2010 itakuwa siku ya kuwachagua viongozi wetu wa kisiasa yaani Madiwani, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania. Mchakato huu wa Uchaguzi Mkuu umekwishaanza kwa kuboresha Madaftari ya wapiga kura na Vyama vya Siasa kuteua wagombea wao katika nafasi hizo zitakazopigiwa kura. Kisha kutakuwa na uteuzi rasmi wa Wawagombea utakaofanywa na Tume ya Uchaguzi Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zikifuatiwa na kampeni, kupiga kura na kutangazwa matokeo.

TUNAWAPONGEZA wale wote ambao wamefanikisha hatua za awali kwani hatua hizo zimefanyika kwa amani. Hata hivyo, tunahimiza kuwa dosari zilizojitokeza (tuhuma za utoaji rushwa na baadhi ya watu kutokubali matokeo na kuandamana) zitazamwe na kushughulikiwa ili zisije zikaleta migogoro yenye kuleta madhara ya kuteteresha amani na umoja wetu wa kitaifa wakati na baada ya mchakato wa uchaguzi .

Vile vile sisi viongozi wa Dini tunampongeza Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Viongozi wa vyama vya CCM na CUF huko Zanzibar (Mheshimiwa Rais Aman Abeid Aman Karume na Katibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad) kwa kufikia muafaka wa kisiasa.Kadhalika tunawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uamuzi wa kuridhia kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Tunaomba Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine kuendelea kuelimisha wananchi juu ya aina hii ya serikali. Vile vile tunataka wale watakaohusika katika uundaji wa serikali hii mara baada ya Uchaguzi Mkuu, waiunde kwa dhati na uzalendo ili iweze kufanya kazi iliyotarajiwa ya kudumisha amani na kuleta maendeleo.

Pamoja na hayo, tunalishukuru Bunge letu la Jamhuri ya Muungano na Serikali yetu kwa kupitisha na kuweka Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Matumizi ya fedha yasiyo halali kwa ajili ya kupata kura yalikuwa kero kwetu na mara nyingi yaliweka madarakani baadhi ya watu wasiokuwa na sifa za uongozi bali utajiri wao. Kinachotakiwa sasa ni kuitekeleza na kuisimamia kikamilifu sheria hii. Hata hivyo, sheria hii haijafahamika kwa wananchi wa kawaida. Hivyo itolewe elimu ya kutosha juu ya sheria hii ili kutoa mchango mkubwa katika ufanisi na utekelezaji wake.

TUNAWAOMBA wale wote waliojiandikisha kufuatilia kampeni za uchaguzi za wagombea wa vyama vyao vya kisiasa ili wafahamu sera na mipango ya wale watakaoifanya kama wataingia madarakani. Ikifika siku ya kupiga kura waende kupiga kura wakijua kwanini wanampigia mgombea huyo au chama hicho cha kisiasa. Wakati wa kupiga kura, tumpigie mgombea mwenye sifa zifuatazo:

· Awe mcha Mungu

· Anayewajali na kuwastahi watu

· Anayependa haki na kuwajali wanyonge

· Awe anaijua na kuitetea Katiba ya nchi

· Awe mkweli kwa maneno na matendo

· Anayeshirikiana na wote bila ubaguzi

· Awe mwenye uwezo wa kuongoza na upeo mpana

· Awe mpenda amani na utulivu

· Awe mwadilifu

· Awe na moyo wa uzalendo yaani anayelipenda taifa lake

TUNAWATAHADHARISHA kuwa uamuzi wa kuchagua chama au mgombea usivutwe na rushwa, udini, kabila au sehemu anayotoka. Vyama vya Siasa au mgombea visijaribu/ asijaribu kutumia hayo katika kuvutia wapiga kura. Viongozi wa Dini kushabikia waziwazi Chama cha Siasa au mgombea ni hatari. Atawagawa waamini kitu ambacho kinaweza kuleta vurugu na mgawanyiko katika eneo husika na pia kitaifa.Viongozi wa Dini wasiruhusu nyumba au sehemu za Ibada kutumika kwa ajili ya mambo ya kisiasa.

Matumizi ya Vyombo vya Habari kwa manufaa ya kibinafsi ni hatari kwa taifa letu. Vyombo hivyo vizingatie maadili mema pasipo kupotosha habari. Habari zisizo na ukweli zinaweza kuchochea chuki na vurugu.

TUNATOA WITO kwa Vyama vya Kisiasa, Wagombea, na vyombo vyote vinavyohusika katika uchaguzi mkuu zikiwemo serikali zote mbili zihakikishe kwamba uchaguzi unakuwa huru na wa haki. Hii itawezekana tu endapo maadili ya uchaguzi yanazingatiwa na kutekelezwa kwa hiyo tunawaasa toeni ahadi zinazotekelezeka. Epukeni jazba, kampeni za kashfa na vurugu. Hii itawapa fursa wapiga kura kufanya uamuzi bila woga na ulio sahihi kwa manufaa ya nchi. Pia itawapa nafasi vyombo vinavyosimamia uchaguzi kusimamia kwa makini zaidi. Kama taratibu zitafuatwa basi matokeo ya uchaguzi yataonyesha matakwa ya wananchi na kukubalika na wadau wote. Ikiwa kutakuwa na dosari yoyote basi taratibu zilizowekwa zitumike na sio vurugu.

Ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu:

· Viongozi wa Dini tutajitahidi kukutana na Viongozi wa Vyama vya Siasa ili kutoa rai yetu na kuwakumbusha wajibu wao wa kuhakikisha kuwa taratibu zote zinafuatwa na pale kutakapokuwa na jambo linalotishia amani juhudi za makusudi zitumike ili kulikabili na kuweka mambo sawa.

· Tutawaelimisha na kuwahamasisha wapiga kura kuhudhuria kampeni, kupiga kura na pasipo kushabikia vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Tunawahimiza waumini wa dini zote kuombea uchaguzi wenye Amani.

No comments:

Post a Comment