Tuesday, June 15, 2010

Mke wa Manyerere awania udiwani

Na Mwandishi Wetu


KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Joyce Manyerere, ametangaza nia ya kuwania udiwani Kata ya Kwembe, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Joyce ambaye ni maarufu kwa jina la Mama Manyerere kwa sasa ni Mjumbe wa Nyumba Kumi, Shina namba 27 Kwembe Kati. Anakuwa miongoni mwa wanachama kadhaa wa CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huuu.

Akitangaza nia yake, Joyce alisema anawania udiwani wa kata hiyo mpya ili aweze kushiriki vema katika kuleta majibu ya changamoto zinazowakabili wana Kwembe.

Pamoja na kusifu kazi kubwa na nzuri iliyofanywa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005-2010, alisema bado kuna changamoto zinazohitaji uongozi madhubuti ili kuzikabili.

“Kwembe bado kuna tatizo kubwa la maji, kuna tatizo barabara, kuna matatizo la ardhi-wananchi wanalalamika, hawa wanahitaji uwakilishi makini na ulio karibu ili kuhakikisha kero za aina hii zinatatuliwa.

“Kwembe sasa kuna vijana wengi waliojiajiri na walioajiriwa katika shughuli kama za udereva wa pikipiki, hawa wanahitaji msukumo mpya wa kuwaunganisha ili waweze kunufaika na vyama vya akiba na mikopo ili siku moja wasiwe waajiriwa tu, bali nao waajiri.

“Kwembe tunahitaji msukumo mpya ili kuhakikisha huduma kama za umeme zinasogezwa karibu zaidi na wananchi, Serikali yetu ina dhamira ya kufanya yote haya, kinachotakiwa ni kuwa na kiongozi (diwani) mwenye kusukumwa na dhamira katika kuwahudumia wananchi,” alisema Joyce ambaye ni mke wa mwanahabari nguli, Manyerere Jacton.

Aidha, Joyce alisema changamoto nyingine ni kuhakikisha kina mama wanajikomboa kiuchumi, hasa kwa kuzingatia kuwa sasa kuna fursa nyingi zinazotolewa na Serikali pamoja na asasi zisizo za kiraia.

“Kina mama ndio walezi wa familia, hawa wakijikomboa kiuchumi, kwa kushirikiana na familia zao wanaweza kabisa kubadili maisha yao na ya jamii nzima ya wana Kwembe.

“Haya yatawezekana vizuri kama miundombinu ya barabara itaboreshwa na hivyo kufanya maeneo mengi ya Kwembe yaunganishwe na sehemu nyingine za jiji au maeneo jirani ya Mkoa wa Pwani,” alisema.

Joyce kitaaluma ni mhasibu. Pia ana stashahada ya Uhusiano wa Kimataifa. Amekuwa mwanachama wa CCM kwa miongo kadhaa sasa, akishika nafasi kadha wa kadha. Ameshakuwa kiongozi wa Nyumba Kumi eneo la Butiama-Msasani, Bonde la Mpunga; hatua iliyomfanya awe Mjumbe wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Alishiriki vilivyo kuwatetea wakazi wa Kijiji cha Butiama-Msasani hadi wakaweza kupata haki kwa maeneo yao yaliyokuwa yamechukuliwa kwa hila na baadhi ya wafanyabiashara.

Ameolewa na ana watoto wawili – Tagazi (msichana) na Simbambili (mvulana).

2 comments:

Anonymous said...

Anapendeza jamani mpeni kura

Anonymous said...

Mbona huyu ni Rhoida Andusamile wa TBS? au mapacha?

Post a Comment