Thursday, May 21, 2009

Nukuu kutoka Busanda

Shahada zote ambazo wananchi wanazo kwa mujibu wa sheria ni mali ya NEC, sasa inakuwaje chama fulani kipite na kuandikisha upya majina na namba zake...hii ni kazi ya tume tu kwani hata mwongozo ndivyo unavyoonyesha,” alisema Msimamizi wa Uchaguzi katika jimbo la Busanda, Dani Mollel kuhusu dai la kunaswa kwa makada wawili wa CCM wakifanya kazi ya kuandikisha shahada za wapiga kura.

"Jimbo ni mali ya CCM na tutalitetea kama Yanga walivyotetea ubingwa wao kwa kutwaa kombe kabla ya ligi kumalizika. Wanachama wakae mkao wa kugombea kiti cha jimbo hilo," alisema katibu mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.

"Huyo ni mganga wa kienyeji," alisema Dk. Slaa alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli ya Makamba kuwa tayari jimbo hilo ni mali ya CCM

Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Samwel Malecela.

"Ni ukweli usiopingika kwamba ndani ya chama changu kuna baadhi ya wananchama na viongozi wanaojihusisha na ufisadi, lakini si wote,” alisema Mama Kilango Malecela, mbunge wa CCM jimbo la Same Mashariki.

Asiwadanganye mtu kwamba ndani ya CCM kuna kiongozi mwenye ujasiri wa kupambana na ufisadi. Maana wameanza kujitokeza baadhi ya wabunge wa CCM eti wakijifanya na wao wana uchungu na nchi hii. Eti na wao wanapambana na ufisadi. Waulizeni walikuwa wapi miaka yote hii nchi ikiuzwa?" aliuliza Zitto Kabwe, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

"Jamani kushindwa ni kubaya, mwenzenu Tarime nilionja ubaya wake mpaka ilibidi nitoroshwe na Green Guard ili kuepuka kuzomewa, sasa tusiposhikamana mambo yatakuwa magumu tutoe tofauti zetu," alisema Katibu Mkuu wa CCM, Ysufu Makamba.

Baadhi ya mafisadi waliopo ndani ya chama chetu ndio wanaoeneza propaganda kwenye vyombo vya habari ili CCM ishindwe," amelalamika Makamu Mwenyekiti msataafu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Bw. John Malecela kuwa chama chake kinahujumiwa na mafisadi kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge na makada wake.

Watakuja, kina Dk. Mwakyembe kuwaambia wao wanapambana na mafisadi, lakini hao ni wanafiki, na wao ni mafisadi tu, kwani huwezi kusema unapambana na ufisadi halafu ukiwa ndani ya CCM,” alisema Zitto.

"CCM kwa kumteua Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Tanzania Bara, John Malecela, anayefahamika zaidi kwa jina la Tingatinga kuwa, ni kumdhalilisha kwa sababu kwa umri wake na wadhifa wake hapaswi kufanya kazi ya kugawa chumvi na magodoro kwa wapiga kura ambao wamekwishaonyesha nia ya kutokichagua chama anachokitetea," alidai Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

"Wale waliotoroka makwao na kukimbilia mijini wakidhani kuwa Serikali ya CCM itakuwa ikimwaga fedha barabarani na wao waokote ndio wanaolaumu na kuunga mkono upinzani lakini wale wenye shughuli zao bado ni wana-CCM," alisema Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa CCM , Bw. Tambwe Hiza.

Napenda kuwaambia ndugu zangu, leo nimewaita hapa kutaka kuwaambia kwamba, tuna kazi moja tu ya kuhakikisha mnachagua CCM katika uchaguzi ujao, sasa nawaambia kama hamtafanya hivyo, tutahakikisha tunawanyang’anya leseni kwani CCM ndiyo yenye serikali,” alisema Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akiongea na wachimbaji wadogo wadogo. “Moja ya mkakati ambao tumeandaa ni kwamba kama CCM haitashinda, TRA itakuja hapa kwa ajili ya kuhakiki kama kweli mnalipa kodi ya mapato, ikiwa ni kinyume chake mtashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya serikali,” aliongeza Ngeleja.

Tumeshangazwa na kauli ya Ngeleja na ndiyo maana tuliamua kumkimbia ndani ya ukumbi, kwa sababu inaonekana wazi kwamba sasa anataka kutufanya Watanzania ni wajinga wa kutupwa, kwanini kaja wakati wa kampeni kututisha hivi?” alihoji mmoja wa wachimbaji hao, Swedi Mussa.

Tumekuwa watu wa kudanganywa kila mwaka sisi… tumeahidiwa umeme hapa miaka mingi, leo tena mnakuja na sera eti ya kuwachagua, tunasema kila jambo lina mwanzo na mwisho wake,” alisema Mayalla kwa niaba ya wafanya biashara wa Katoro.

Nasikia kuna Chopa linakuja, sisi tunaondoka, lakini mjue kuwa sisi wana CCM tuna uwezo wa kuleta ndege Boeing hata kumi,” alisema Salum Msabaha, Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma katika mkutano huo wa kumnadi mgombea wao, Bukwimba.

Nawaomba mfanye kazi yenu vizuri,” alisema Mbunge wa Nyamagana, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, akiwa ndani ya gari lenye namba za Ubalozi wa Afrika Mashariki, huku akiwa amevalia fulana ya rangi ya njano na kijani, akitoa agizo kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na silaha mbalimbali, zikiwamo za moto waliojiandaa kwa mapambano, wakiwa wamepiga kambi jirani na viwanja hivyo (kulikotarajiwa kutua helikopta).

Usinione hivi sina raha, kwanza usiku silali wala sipati usingizi nafikiria Busanda, lakini nitahakikisha kampeni zinafanyika kwa amani kubwa na vurumai zitakoma tu,” alisema Kaimu Kamanda wa polisi, Kalinga. ( Licha ya hivyo vijana wa CCM wameendelea kutembeza mkong'oto kwa wananchi bila wasi wasi)

Chanzo: Jamii Forums