Saturday, June 27, 2009

Sheikh Gorogosi Afa Ajalini

Breaking News
Taarifa mbazo bado ni moto ni kwamba Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheik Suleiman Gorogosi amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea kwenye Kijiji cha Mnolela Wilaya ya Lindi Vijijini baada ya tairi ya mbele ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Mtwara kupasuka na kupinduka.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Sifuel Shirima zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 8:09 katika barabara ya Mtwara-Lindi wakati akitokea Uwanja wa Ndege Mtwara baada ya kushuka kwenye ndege akitoa jijini Dar es Salaam.

Kamanda Shirima alisema katika gari hilo kulikuwa na watu watatu, akiwamo Bakari Maguo, mfanyabiashara wa Lindi ambaye ni mmiliki wa gari hilo na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Lindi mjini, Bakari Fundi ambao wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Ligula mkoani Mtwara.

Gorogosi alikuwa amekwenda Lindi kufungisha ndoa ya mtoto wa Maguo ambaye ni mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambayo ilikuwa ifungwe leo.

Ndugu wa marehemu Abilahi Mohammed aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa mazishi wa Gorogosi ambaye alikuwa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Lindi yatafanyika saa 10:00 jioni leo jioni mjini humo.

Pia Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), lilitoa taarifa jana jioni likieleza kuwa Gorogosi lilithibitisha kifo cha Gologosi na kueleza kuwa atazikwa leo.
Marehemu ameacha wake wawili. Kabla ya kifo chake alikuwa pia mjumbe wa baraza la Ulamaa la Bakwata.

No comments:

Post a Comment