Rais Jakaya Kikwete amehutubia taifa kupitia kwa wazee wa Mkoa wa Dodoma na wabunge. Amezungumzia zaidi msukosuko wa uchumi duniani kwa mapana yake na hali ya uchumi kwa ujumla; na overview ya bajeti. Kwa namna fulani, ni kama ame-pri-empty hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha ya kesho cheki hapa. JK ameibua kitu kipya cha serikali kudhamini madeni ili kupunguza makali ya uchumi wa dunia. Mdau kanitumia SMS akihoji, je, hiyo si EPA nyingine? Reuters wameandika hivi na Hotuba Kamili Hii Hapa.
Wakati huo huo, Kurugenzi ya Mwasiliano Ikulu imesema yafuatayo: Mambo makuu katika Hotuba ya Rais, Dodoma, – jumatano, Juni 10, 2009.
1. Rais ameelezea hali ya mtikisiko wa uchumi duniani, chimbuko la mtikisiko huo na athari za hali hiyo kwa uchumi wa Tanzania. Athari hizo ni kama ziafuatazo:
(a) Bei na mahitaji ya bidhaa za Tanzania kwenye masoko ya kimataifa yamepungua.
(b) Mahitaji na bei za madini ya vito vimepungua kwenye masoko ya kimataifa
(c) Mahitaji ya mazao ya kilimo ya Tanzania kama vile maua na mboga yamepungua kwa asilimia 25
(d) Viwanda vya ngozi, nguo, nyuzi na mavazi pia vimeathirika na hivyo kuathiri pia upatikanaji wa ajira nchini
(e) Sekta ya utalii ambayo ndiyo kubwa kwa uingizaji wa fedha za kigeni pia imeathirika kwa watalii wanaokuja nchini kupungua
(f) Mapato ya Serikali pia yamepungua na hivyo kuathiri mapato ya ndani na mapato ya fedha za kigeni
(g) Uwekezaji kutoka nje umepungua pia na baadhi ya makampuni yaliyokuwa yanataka kuja kuwekeza Tanzania, ama yameahirisha ama yamefuta mipango yao ya uwekezaji. Mifano ni mradi wa uwekezaji katika nickel pale Kabanga, Ngara, Kagera na miradi ya umeme, saruji, mbolea na aluminium smelter mkoani Mtwara
(h) Hali ya ajira nchini imekuwa mbaya zaidi kwa sababu ya matatizo hayo ya uchumi na hadi Aprili, mwaka huu, kiasi cha watu 48,000 walikuwa wamepoteza ajira
(i) Vile vile kasi ya kukua kwa uchumi wa Tanzania inakadiriwa kuwa itapungua kutoka kwenye asilimia 7.4 kama ilivyobashiriwa mwaka huu hadi kufikia asilimia 5 hadi 6.
2. Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete ametangaza mkakati wa kuhami na kunusuru uchumi wa Tanzania kwa malengo makuu manne yafuatayo:
(a) Kulinda ajira na vipato vya wananchi
(b) Kuhakikisha upatikanaji wa chakula
(c) Kulinda uwekezaji muhimu katika miradi ya maendeleo, hususan miundombinu
(d) Kulinda programu muhimu za kijamii
3. Kutokana na hali hiyo, Rais ametangaza hatua zifuatazo katika kutekeleza mkakati huo wa kuunusuru uchumi (rescue package):
(a) Serikali imeamua kufidia hasara waliyopata wanunuzi wa mazao kwa msimu uliopita wa 2008/2009. Hasara hiyo ni kiasi cha bilioni 21.9 na Serikali italipia hasara hiyo ambayo imetokana na kushuka ghafla kwa bei ya mazao ya Tanzania kwenye soko la kimataifa
(b) Serikali itatoa udhamini kwa kuahirisha mikopo ya walioathirika ambao ni pamoja na viwanda, utalii, kilimo na sekta nyingi za uchumi kwa muda wa miaka miwili. Serikali imeyataka mabenki kutokutoza riba kwenye mikopo hiyo katika miaka hiyo miwili
(c) Serikali itatoa mitaji ya uendeshaji (working capital) kwa riba nafuu na itayakopesha mabenki kwa riba ndogo ya asilimia mbili na mabenki hayo yatatakiwa kuwakopesha wahitaji kwa riba ndogo zaidi kuliko ilivyo sasa.
(d) Serikali imedhamiria kuboresha mifuko ya dhamana ikiwa ni pamoja na mifuko ya kukopesha biashara ndogo ndogo kwa kuiongezea fedha zinazoweza kukopwa na wananchi
(e) Serikali imeamua kuongeza kasi ya uzalishaji chakula kwa kutoa mikopo ya thamani ya bilioni 20 kupitia Benki ya TIB, na pia kutoka kiasi kingine cha sh bilioni 20 kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya ununuzi wa zana za kilimo kupitia taasisi za karadha, na kuongeza idadi ya wakulima watakaopata mbolea ya ruzuku na kiasi cha bilioni 90 kwa ajili ya mboleo hiyo. Vile vile, Serikali imeamua kuanza kuutumia Mfuko wa Hifadhi ya Chakula (SGR) kupunguza bei ya vyakula kwa wananchi na hifadhi hiyo itaongezewa fedha za kununulia chakula zaidi
(f) Serikali imeamua kukwamua mradi wa kusambaza umeme mkoani Mtwara na pia kuboresha Reli ya Kati kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 43.
(g) Serikali imeamua kuhakikisha kuwa programu zote za kijamii kama maji, elimu na afya kama vile ya kupambana na magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu na malaria haziathiriki kwa sababu ya msukosuko wa sasa wa kiuchumi.
(h) MPANGO wote huu utaigharimu Serikali kiasi cha sh bilioni 1, 692.5 (karibu sh trilioni 1.7). Fedha hizo zimetengwa katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2009/2010 inayoanza Julai Mosi, 2009.
Sehemu kubwa ya fedha hizo ni za ndani ya nchi ingawa kutakuwapo na michango ya wabia wa maendeleo kama Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF), Serikali ya India na Umoja wa Ulaya (EU).
No comments:
Post a Comment