Thursday, November 10, 2005

Sasa Yamekuwa. Wengi Wasubiri Sura ya Nyerere

SHAUKU kubwa imetawala wakazi wa Dodoma. Wengi wanataka kuona ile sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyowekwa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya kiongozi huyo inavyofanana.
Mwaka jana sanamu kama hiyo iliwekwa mjini Mwanza na nyingine Tanga, lakini wakazi wa miji hiyo walisema hazifanani na sura ya Mwalimu. Sasa ile ya Dodoma inafunguliwa kesho na Waziri Mkuu Frederick Sumaye. Je, itafanana na Nyerere?
Sanamu lenyewe, lilitengenezwa nchini Korea Kaskazini kwa sh 200 milioni na kufungwa na Wakorea wenyewe takriban tatu zilizopita, katika uwanja (Nyerere Square) uliojengwa kwa zaidi ya sh 500 milioni.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Alhaji Mussa Nkhangaa, ilithibitisha jana kuwepo kwa tukio hilo na kuraja lengo lake kuwa, ni kuweka kumbukumbu ya Taifa ya kudumu ya Mwalimu Nyerere kama mwasisi wa taifa na pia mwasisi wa Wazo la Kuhamishia Makao Makuu ya serikali Dodoma.

3 comments:

Indya Nkya said...

Sanamu imetengenezwa Korea? Oh! hivi inahitaji utaalam wa hali ya juu sana kiasi kwamba hapo Tanzania haiwezekani ehe? Basi utupashe ikishafunguliwa ili tujue kweli kulikuwa na ulazima wa kutengenezewa Korea!!

Mija Shija Sayi said...

Kama ingetokea Mwalimu kufufuka ghafla na kukuta ame enziwa kwa sanamu kama kumbukumbu yake, nina uhakika angefurahi sana, lakini furaha yake ingekoma ghafla pale ambapo angegundua kuwa sanamu ile haikutengenezwa na wananchi wake aliowapenda kwa moyo wake wote, bali huko Korea tena gharama ambayo ingeweza kununua madawati, madawa na pembejeo kwa wananchi. Bila shaka angesema......"ndio maana nilikuwa nashangaa?....iweje watu wangu wanaonijua fika watengeneze mfano wa sanamu yangu?...lakini sasa nimejua kwa nini... !!!!". Hivi jamani ni nani ambaye hajui kwamba Mwalimu hakuhusudu kabisa mambo ya kubabaikia watu wa nje? maana hata alipozidiwa wakati akiumwa ilikuwa mbinde kumshawishi kwenda kutibiwa Ulaya, alitaka atibiwe hapa hapa, sasa kama kweli tunafuata nyayo zake iweje sanamu yake itengenezwe ughaibuni?

FOSEWERD Initiatives said...

hayo ni matumizi mabaya ya hela za umma! ndo yale yale tulikuwa runasema! tumesamehewa madeni! - sahihi lakini awali ya yote, hizo hela zilifanya nini?

Post a Comment