Wednesday, August 11, 2010

Hakimu atishia kufuta kesi ya MuroNa Rabia Bakari

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Bw. Gabriel Mirumbe anayesikiliza kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Bw. Jerry Muro na wenzake wawili, amekuwa mbogo, akakataa maombi ya kuiahirisha na kutishia kufuta kesi hiyo.

Hatua hiyo ilitokea mahakamani hapo jana, wakati upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Bw. Zuberi Mpakatu ulipoomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kutokana na baadhi ya mambo kutokamilika.

Wakili Mpakatu aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikwenda kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashahidi, na kwamba walikuwa na shahidi mmoja, lakini wanaiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kutokana na baadhi ya mambo kutokamilika, kwa vile Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Boniface Stanlaus anayeendesha kesi hiyo yuko likizo.

Akijibu kwa ukali hoja hiyo, Hakimu Mirumbe alisema hataki kuahirisha kesi hiyo, na kama hawataki kuendelea na kesi ataifuta.

"Nawapa nusu saa mwende mkajipange, na mrudi hapa tuendelee na kesi, la sivyo nafuta kesi hii," alisema Bw. Mirumbe.

Baada ya nusu saa kesi hiyo iliendelea kwa shahidi kuanza kutoa ushahidi wake, lakini muda mfupi baadaye Hakimu Mirumbe alimkatisha kutoa ushahidi kwa madai kuwa upande wa mashtaka haujafuata taratibu za kimahakama.

Shahidi huyo, Sajenti Peter Jumamosi alijitambulisha kuwa anatokea Ofisi ya Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, na kudai kuwa anakumbuka Februari Mosi mwaka huu, bosi wake Bw. Charles Mkumbo aliingia ofisini akiwa na watu wawili.

"Nilipewa mmoja kwa ajili ya kumfanyia mahojiano na mwingine alipewa mwenzangu, ambapo mimi nilipewa mshtakiwa wa tatu."

Kabla hajaendelea alikatizwa na hakimu, huku akiutaka upande wa mashtaka kuwa na maelezo ya onyo, ambapo upande wa mashtaka ulidai maelezo hayo anayo askari ambaye hata hivyo hakupatikana mapema.

Ndipo hakimu Mirumbe alipoendelea kulalamika na kudai kuwa lazima taratibu za mahakama zifuatwe, na kumtaka shahidi huyo kushuka kizimbani na kuacha kutoa ushahidi.

"Kwanza niliwaambia mhakikishe mnakuja na mashahidi watano wako wapi? Sipendi kupoteza muda," aliongeza.

Baada ya maelezo hayo, hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi leo, ambapo itaendelea kusikilizwa.

Awali wakili huyo wa Serikali Mkuu, Boniface Stanslaus akishirikiana na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Ben Lincoln, alidai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hayo Januari 29, 2010.

Wakili Stanslaus alidai kuwa washtakiwa hao pamoja na wenzao wengine ambao hawajafikishwa mahakamani walitenda makosa hayo ya kula njama na kuomba rushwa kinyume cha kifungu cha 15 (1)(a) cha Sheria ya Kuzia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Stanslaus alidai kuwa Muro aliomba rushwa hiyo kutoka kwa Bw. Wage katika Hoteli ya Sea Cliff wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ili asitangaze habari zake zinazohusiana na matumizi mabaya ya fedha za umma.

mwisho

No comments:

Post a Comment