Wednesday, July 14, 2010

CCJ yahamia Chadema

Kuna taarifa kuwa vigogo wa juu wa Chama cha Jamii wamehamia Chadema. Waliotajwa kwa haraka ni Msemaji, Fred Mpendazoe na Mwenyekiti, Richard Kiyabo. Taarifa zaidi baadaye.


TAMKO LA VIONGOZI WA CHAMA CHA JAMII (CCJ) KUWATAKA WANACHAMA WA CCJ WAGOMBEE NAFASI ZA UCHAGULIWA
KATIKA UCHAGUZI MKUU UJAO KUPITIA CHADEMA

UTANGULIZI

Ndugu Viongozi, Wanahabari, Wanachama na Wananchi kwa ujumla.
Tunayo furaha kubwa isiyo na kifani, kwa kuungana nanyi katika
mkutano huu ambao unaandika historia mpya yenye kuleta mabadiliko
ya kweli katika taifa letu la Tanzania. Historia ambayo itakumbukwa
kizazi hata kizazi, historia itakayowafanya Watanzania wajivunie na
kuifaidi nchi yao.
Ndugu zangu kabla sijaeleza nini kimetuleta hapa, napenda
kuwarudisha nyuma kidogo. January 18 mwaka huu sisi wananchi
wazalendo tulikutana jijini Dar es Salaam kutekeleza wajibu wetu
kikatiba wa kuunganisha mawazo yetu pamoja na kuunda chama cha
siasa kwa jina la Chama Cha Jamii (CCJ).
CCJ kilizingatia changamoto zote zinazoikabili nchi yetu tangu na
baada ya uhuru na kilibeba matarajio ya wananchi wa leo na kesho,
kikiwa na lengo kuu la kuleta mageuzi ya kitaifa ya kidemokrasia,
kiuchumi, kijamii, na kisiasa kwa faida yetu sisi sote na vizazi vijavyo.

USAJILI WA MUDA

Mwezi huo huo CCJ ilipeleka maombi ya usajili wa muda katika ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Na baada ya urasimu wa hapa na
pale, hatimaye Machi 3, 2010 CCJ ilipata cheti cha usajili wa muda. Hii
ilikuwa ni hatua ya mwanzo kabisa ili kiweze kuanza shughuli za
kutafuta wanachana na hatimaye kikitimiza masharti yaliyopo kwa
mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992, kiweze kupewa usajili
wa kudumu.
Hata hivyo, toka mwanzo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini,
imekuwa ikionyesha nia yake waziwazi ya kutotaka kukipa CCJ usajili
wa kudumu hata kama kitatimiza masharti. Ndani ya siku si chini ya
sabini (70), CCJ kilikamilisha masharti yote na kupeleka maombi ya
usajili wa kudumu. Msajili kupitia vyombo vya habari kwa mara nyingine
aliweka wazi nia yake ya kutotoa cheti cha usajili wa kudumu kwa CCJ.
Ndugu wananchi, kutokana na shinikizo toka kwa watanzania wenye
uchungu na nchi hii na wenye kutaka kuona mabadiliko, pia shinikizo
toka kwa ofisi za kibalozi zilizopo nchini, chama cha wanasheria tawi la
Arusha bila kusahau wanachama wa CCJ, hatimaye tarehe 3/5/2010
msajili kwa shingo upande aliamua kufanya uhakiki wa wanachama wa
CCJ kwa mikoa minne akianzia Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na
baadaye Mjini Magharibi.
Ndugu zangu nyote ni mashahidi wa hujuma tulizofanyiwa kiasi cha
kupelekea kusitishwa kwa zoezi zima la uhakiki. Na kwa kuwa nia ya
msajili ilikuwa ni kuichafua CCJ, alitangaza kuwa CCJ-Dar ina
wanachama 13 tu, na licha ya kuwa tulimwandikia barua ya kusitisha
zoezi la uhakiki bado aliendelea na Pwani kisha kutoa tamko kuwa
CCJ-Pwani haina hata ofisi licha ya wanachama. Baadaye akasema
Zanzibar tuna mwanachama mmoja, yote haya aliyafanya kwa
makusudi ili CCJ ionekane si kitu.
Msajili ameonyesha dharau na kejeli za wazi kwa watanzania,
tungependa kuwafahamisha Watanzania kwamba, wananchi wengi
sehemu mbalimbali za nchi yetu watu wa kila rika, dini mbalimbali
wakiwepo wasanii, wakulima, wafanyakazi pamoja na wastaafu
wamekikubali na kukipokea Chama Cha Jamii na wengi wamejiunga.
Tarakimu zilizopo ofisini, mpaka sasa kuna watanzania takriban 9500
wamejiunga na CCJ. Aidha wapo watanzania nje ya nchi kama vile
Marekani, Japani, Uingereza, Korea ya Kusini na Afrika Kusini
waliojiunga na CCJ.
Watanzania hawa waliojiunga na CCJ, aidha walifika wao wenyewe
ofisini au walishawishiwa na wananchi ambao walikuwa tayari
wamejiunga awali ukiondoa wanachama 102 walio jiunga kwenye
mkutano wa hadhara wa kuompokea Mh Mpendazoe uliofanyika pale
Mwembeyanga.

KUGOMBEA KUPITIA CHADEMA

Kwa mda mrefu kumekuwa na mazungummzo kati ya CCJ na
CHADEMA ya kuwa na ushirikiano na hususan katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika oktoba 2010, hii inatokana na ukweli kuwa vyama hivi
vina itikadi na mwelekeo unaofanana. Ushirikiano huu ungeendelea
hata baada ya CCJ kupata usajili wa kudumu. Sasa, kwa kuwa muda
tuliobaki nao ni mchache kwa CCJ kupata usajili wa kudumu na
kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea uchaguzi mkuu, hivyo basi,
tunatoa wito kwa wanachama wa CCJ wenye sifa na nia ya kugombea
nafasi za uongozi wa kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao,
kugombea kupitia CHADEMA.
Ndugu zangu tunafanya hivi si kwa maslahi yetu au ya vyama vyetu,
isipokuwa tunafanya hivi kwa maslahi ya Taifa. Ndio maana tumeamua
kuachia nyadhifa zetu na kujiunga CHADEMA kama wanachama wa
kawaida. Hivyo basi, tunawaomba wanachama wote wa CCJ bila
kusahau wote wenye mapenzi mema na taifa hili, kuunga mkono
maamuzi haya na kuwachagua wote watakaosimamishwa na
CHADEMA.
Kwa kuwa CCJ tunaamini kuwa Umoja ni Nguvu ya pekee ya wananchi
katika kujenga Usawa na Uhuru na katika kuondoa Umaskini, Ujinga,
Maradhi na kupambana na Ufisadi, na kwa kuwa CHADEMA kinaamini
katika falsafa ya Nguvu na Mamlaka ya Umma ambayo inalenga katika
kuwaamasisha, kuwaelimisha, kuwashawishi na kuwandaa Watanzania
wachukue hatua kuimiliki, kuitawala, kuilinda na kuifaidi nchi yao, hivyo basi tunatangaza rasmi kuwa Dickson Ngihily (Naibu Katibu Mkuu-Bara), Richard Kiyabo (Mwenyekiti-Taifa) na Fred Mpendazoe (Msemaji-Taifa) watagombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya CHADEMA mara baada ya kuchukua kadi zao za uanachama wa CHADEMA.
Ndugu zangu nyote ni mashahidi na mnaelewa juu ya utajiri mkubwa
ambao Mwenyezi Mungu ameuweka ndani ya mipaka ya Tanzania.
Hata hivyo ni jambo la kusikitisha kuwa wananchi wake ni maskini wa
kutupwa, hiki ni kitendawili ambacho jibu lake ni la kusikitisha kwani jibu ni dhahiri, ni kutokana na uongozi usiojali wanyonge na usio na
uzalendo wa CCM.
Ni dhahiri kwamba watanzania wamechoshwa na hali hii na wanahitaji
mabadiliko ya kweli katika uongozi na uendeshaji wa nchi, hii ni
kutokana na ukweli kuwa CCM na serikali yake haviwezi kuleta
mabadiliko hayo na kamwe haitaweza. Ni dhahiri kwamba watanzania
wamechoka kuishi maisha yasiyo na matumaini, maisha yasiyo na
mwelekeo wa kesho, hivyo mabadiliko yanahitajika.
Na hili ndilo tumaini letu na tena hii ndiyo imani tunayoondoka nayo
kuwa sote kwa pamoja tunahitaji mabadiliko ya dhati na kwa
ushirikiano huu Tanzania yenye neema bila CCM inawezekana! Huu
sio wakati wa kupigishwa porojo na kupewa kanga na Tshirts, ni wakati
wa kusimama pamoja wanaume kwa wanawake, vijana na watoto
kudai mabadiliko katika sanduku la kupigia kura. Narudia tena
Tanzania yenye Neema Bila CCM inawezekana.
Mungu ibariki Tanzania
Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment