Tuesday, April 13, 2010

ATANGAZA KUMVAA 'VIJISENTI'

Huyu ndiye Bw. Zacharia Fuli Shigukulu aliyetangaza kumvaa Andrew Chenge, alimaarufu Mzee wa Vijisenti, katika kuwania ubunge kwenye jimbo la Bariagi Magharibi. Haya ndiyo maelezo yake:


'Mzee wa Vijisenti' apata mpinzani

Na Suleiman Abeid, Bariadi

MBUNGE wa Jimbo la Bariadi Magharibi mkoani Shinyanga, Bw. Andrew Chenge maarufu kama ‘Mzee wa Vijisenti’ amepata mpinzani ambaye ametangaza rasmi nia yake ya kugombea katika jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Aliyetangaza nia hiyo ya kupambana na Bw. Chenge ni Bw. Zacharia Fuli Shigukulu (pichani) ambaye ni Afisa Mipango katika Shirika la World vision mkoani Dodoma katika miradi ya Sanzawa na Kwamtoro ADP.

Akitangaza nia hiyo jana kwa waandishi wa habari mjini hapa, Bw. Shigukulu alisema ameamua kutangaza rasmi mapema kuwania nafasi hiyo katika jimbo la Bw. Chenge baada ya kutoridhishwa na hali ya maendeleo ya wapiga kura wake ambayo anaamini inatokana na mbunge wao kutokuwa karibu nao.

Bw. Shigukulu alisema yapo mambo manne makuu ambayo yamesababisha aamue kujitosa kupambana na Bw. Chenge likiwemo tatizo kuu la ubovu wa miundombinu katika maeneo mengi ya vijijini, hali ambayo inasababisha ugumu wa wakulima kusafirisha mazao yao katika masoko.

Alisema maeneo mengi ya vijijini katika jimbo la Bariadi Magharibi hayana barabara zinazopitika kwa mwaka mzima na kutoa mfano wa hali ilivyo hivi sasa na kwamba mbunge aliyepo haioni hali hiyo kwa vile, wakati akigombea mwaka 2005 dhamira yake haikuwa kuwasaidia wananchi.

“Huyu bwana kwa kweli hakuwa na dhamira kabisa ya kuwasaidia wapiga kura wa jimbo lake, badala yake aliwakumbatia wafanyabiashara wakubwa, na hawa ndiyo
walimsaidia kushinda, leo hii tembelea vijijini utaona kwa macho hali halisi ilivyo huhitaji kusimuliwa,” alieleza Bw. Shigukulu na kuongeza.

“Sasa kutokana na hali hiyo ndiyo maana wananchi wameniomba na kunisihi nijitokeze kugombea nafasi hiyo. Wanaamini nitaweza kuleta mabadiliko kwa vile sasa wanahitaji mabadiliko, awali nilifuatwa na watu wa chama cha upinzani cha UDP wakaniomba, lakini nilikataa kwa vile mimi ni CCM damu, nikasema nitagombea kupitia chama tawala,”

“Hii inatokana na kuchoshwa na hali ilivyo hivi sasa katika jimbo lao, hali ambayo wamedai wataweka kando tofuati zao za kisiasa ambapo wana-UDP nao wameeleza nia yao ya kuniunga mkono iwapo nitateuliwa kuwa mgombea kwa tiketi ya CCM. Ni jambo ambalo linatoa picha halisi ya jinsi gani watu wa Bariadi Magharibi wanavyohitaji mabadiliko,” alieleza.

Bw. Shigukulu alieleza kuwa mwaka 2005 alishindwa kugombea katika jimbo hilo baada ya kutishwa na kasi ya matumizi makubwa ya fedha zilizokuwa zikitolewa kwa baadhi ya wajumbe wa CCM ikiwemo baiskeli, hali ambayo ilisababisha asitishe nia yake kutokana na uwezo wake mdogo wa kifedha.

Alisema baada ya CCM kufanya mabadiliko makubwa katika upigaji wa kura za maoni ambapo hivi sasa wanachama wote kwa ujumla watahusika badala ya kundi dogo la wajumbe, anaamini demokrasia imepanuka na ataweza kupata kihalali kile alichokikusudia.

“Mwaka 2005 nilitaka kuwania nafasi hii, lakini nilishtushwa na matumizi makubwa ya fedha zilizokuwa zikimwagwa kwa wajumbe, nilisita, lakini baada ya CCM kuamua kupanua wigo katika upigaji wa kura za maoni, ni wazi demokrasia imepanuka hivyo nimeamua kujitosa, na hii sheria mpya ya kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi itasaidia,” alieleza.

Bw. Shigukulu alizaliwa mwaka 1966 katika Kijiji cha Nyanguge kata ya Mha’ngu Bariadi amewahi kufanya kazi katika kampuni ya Business Times Ltd kati ya mwaka 1994 na 1996 akiwa kama Afisa Mauzo Msaidizi, Afisa Utawala na baadaye Meneja Mauzo wa Mkoa wa Dar es salaam .

Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Nyanguge “B” Bariadi, na kisha elimu ya sekondari katika Sekondari ya Shinyanbga (1983 – 1986) na masomo ya kidato cha tano na sita katika sekondari ya Galonos mkoani Tanga.

Mwaka 1989 mpaka 1990 alikwenda Jeshini katika kambi ya JKT Oljoro kwa mujibu wa sheria za wakati huo na baadaye kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam apohitimu mwaka 1994. Pia amepata mafunzo mbalimbali ya kujiendelea kutoka katika vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Ana Shahada ya Uzamili ya Maendeleo kutoka Chuo cha Southern New Hampshire kinachoshirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na moja ya mafanikio yake makubwa akiwa World vision ni kuanzisha Ushirika wa Akiba na Mikopo wa Nankwenda SACCOS ambao ni sasa ni ushirika wa mfano katika World vision Tanzania.

Kujitangaza kwa Bw. Shigukulu kuwania nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo la Bariadi Magharibi kumeondoa minong’ono iliyoanza kujitokeza kuwa huenda Bw. Chenge katika uchaguzi wa mwaka huu angepita bila kupingwa baada ya kundi la baadhi ya wanasiasa kutaka kumtangaza rasmi kuwa ni mgombea pekee.

1 comment:

Anonymous said...

Wacha hizo siasa, sasa hii inatusaidia nini

Post a Comment