Monday, August 10, 2009

Mahanga Katika Mjadala wa Ufisadi

Kadri siku zinavyosogea, tunazidi kujipambanua kujua nani ni nani katika mjadala wa ufisadi. Mtu wa karibuni kabisa ni Mbunge wa Ukonga, Naibu Waziri wa Kazi,
Ajira na Vijana, Dk Makongoro Mahanga aliyekaririwa na Gazeti la Mwananchi Jumalipi akisema:
CCM kuna Mafisadi wanne tu; akimaanisha kuwa si wengi, hivyo hawastahili kiwango cha kelele kinachopigwa dhidi ya ufisadi. Na kuwa kelele hizo 'zinakichafua' chama chao. Leo mjumbe huyo wa NEC katoa taarifa mpya ya kufafanua alichosema jana: Isome kama ilivyotolewa: hapo chini:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KAULI YANGU KUHUSU SUALA LA UFISADI NDANI YA CCM
Katika ukurasa wa mbele wa gazeti la Mwananchi Jumapili toleo Na. 03345 la tarehe 09 Agosti 2009, kulikuwa na habari yenye kichwa cha habari “Mahanga: Mafisadi CCM ni wanne tu”. Habari hii inaeleza na kunukuu mazungumzo yangu na gazeti hilo kuhusu maoni yangu kuhusu mjadala unaoendelea ndani na nje ya Bunge kuhusu suala la ufisadi ndani ya CCM.

Nimesikitishwa na namna mahojiano yangu na gazeti hilo yalivyopewa kichwa cha habari cha kupotosha kabisa. Kichwa cha habari “Mahanga: Mafisadi CCM ni wanne tu” kinapotosha kabisa, siyo tu yale niliyoyasema, lakini pia hakiendani hata na habari yenyewe ilivyoelezwa kwenye gazeti hilo ukisoma habari hiyo nzima.

Kwa mfano, wakati kichwa cha habari kinataka wasomaji waamini kwamba nilisema “…. Kuna mafisadi wane tu CCM’, ukisoma ndani ya habari hiyo inaeleza kwamba nilisema “..Hawa wanaoitwa mafisadi wako wapi? Mbona hawatajwi?...” ‘Tathmini yake inaonyesha kuwa kelele zote za ufisadi zinawalenga watu ambao hawazidi wanne ndani ya chama hicho (CCM), na kwamba miongoni mwao, tayari wameanza kushughulikiwa’. Ni wazi kwamba hata hiyo nukuu ya hapo juu ina tofauti kubwa sana kimantinki na ki-ukweli na kichwa cha habari hiyo kama ilivyowekwa na gazeti hilo.

Huku nikipinga vikali kwamba sikusema hayo yaliyotolewa kwenye nukuu ya kichwa cha habari cha gazeti hilo, ningependa kuweka sawa yale niliyoyasema nilipopigiwa simu na mwandishi wa gazeti la Mwananchi Jumapili, Bw. Leon Bahati, ili kupata maoni yangu kuhusu mjadala huo na nilipoongea na mhariri wa gazeti hilo aliponipigia simu tena baadaye. Aidha napenda kuongezea maoni yangu ya ziada kuhusu suala hilo.

Nilichowaambia waandishi hao kama ilivyoelezwa kwa usahihi kwa asilimia kubwa ndani ya habari yenyewe ni kwambva wabunge na watu wengine ndani ya CCM wanaotamba kupambana na ufisadi na kutoa tuhuma nzito kwamba kuna mafisadi ndani ya chama wanaohatarisha uhai na ushindi wa CCM katika chaguzi zijazo, wanapambana na mafisadi hewa au wa kufikirika kwa kuwa wameshindwa kuwataja hao mafisadi waziwazi au kupeleka ushahidi wao kwenye vyombo vya dola kama TAKUKURU, Mahakama ama kwa Rais.

Nilisema kinachohatarisha ushindi wa CCM siyo hao “mafisadi” wa kufikirika au wa kubuni ndani ya CCM kama hao “wapambanaji” wanavyodai, bali ni kauli hizo za “wapambanaji” ndizo zitakiharibia chama kwani wananchi wasioelewa malengo yao halisi wanaweza kuamini kwamba kweli chama hiki kimejaa mafisadi na kukinyima kura.

Nikasema naamini hii ndiyo nia ya watu hawa wanaojiita wapambanaji wa ufisadi. Kwamba kwa makusudi tu ama kwa wivu na chuki zao za kisiasa wameamua kukiharibia chama chao ili wananchi wasione na kufurahia mambo mazuri na makubwa ya maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya nne ya CCM kwenye sekta za elimu, barabara, afya, maji, kuondoa umasikini na hata hilo la kupambana na rushwa na maovu mengine kwenye jamii, na badala yake wakihukumu chama kwa ufisadi wa kufikirika na uliotiwa chumvi unaoenezwa na hawa “wapambanaji”.

Ni kweli kabisa kwamba rushwa na ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma ni mambo mabaya yanayorudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu, na ni lazima wananchi wote tupambane nayo; na lazima tupongeze juhudi za Rais Kikwete na vyombo alivyoviunda na kuviboresha kama TAKUKURU na Mahakama katika kupambana na maovu hayo, na kama wananchi, ni budi tutoe ushirikiano kwa Rais na vyombo hivi katika mapambano haya, lakini watu wasiofuata utaratibu wa kutoa vielelezo na ushahidi kwenye vyombo husika na kubaki kutoa tuhuma za jumla jumla tu kwenye vyombo vya habari na majukwaa ya kisiasa hawasaidii nchi katika mapambano dhidi ya ufisadi, badala yake wanakuza chuki tu miongoni mwa jamii.

Lakini kibaya zaidi kama hao wanaotoa tuhuma hizo za kufikirika ni viongozi na makada wa CCM na wanatuhumu viongozi na makada wenzao ndani ya CCM bila kutoa ushahidi tena kwenye vyombo vya habari na majukwaa ya kisiasa bila kufuata taratibu za chama za kukosoana na kukemeana ndani ya vikao rasmi vya chama, basi wanakiharibia chama na kusaidia upinzani, na nikasema watu hawa kimsingi si “wenzetu” tena, bali ni wapinzani na ni vyema wakaondoka mapema kwenye chama hiki na kujiunga rasmi na upinzani, kwani wapinzani kushutumu CCM waziwazi ni mbinu za kawaida za siasa za upinzanani duniani.Lakini niliendelea kusema kwamba CCM, kama chama, siyo fisadi.

Inawezekana kuna wanachama wachache wasio waaminifu na wenye maadili mabovu na wala rushwa, lakini hao tuwashughulikie kwa taratibu za kutoa ushahidi na kufuata misingi ya sheria za nchi kama ambavyo watuhumiwa kadhaa walivyokwisha pelekwa mahakamani ambapo kesi zao zinaendelea kisheria.

Hata hivyo nilielezea gazeti hilo kwamba ingawa hawa “wapambanaji” wa ufisadi hawawataji wana CCM wenzao wanaowatuhumu kwa ufisadi, tathmini yangu ya kimazingira inaonyesha kwamba wanawanyooshea zaidi vidole watu wachache tu pengine wasiozidi wanne, siyo kwa kuwa wana ushahidi wa wazi wa ufisadi wao, lakini kwa maoni yangu, ni chuki na wivu tu wa kisiasa dhidi ya watu hao na kutaka watanzania wote warithi chuki na wivu wao dhidi ya watu hao.

Kwa tathmini yangu, sababu ya chuki na wivu huo unatokana zaidi na matokeo ya chaguzi za kitaifa zilizopita na zijazo, ambapo “wapambanaji” katika chaguzi zilizopita walikosa nafasi walizotaka za uongozi na madaraka nchini, na hivyo kujenga chuki dhidi ya hao wanaowaona kuwa ndiyo “king makers”, na kihistoria “king makers” duniani huwa hawapendwi na watu wengi.

Na ndiyo maana nikasema, hivi hata kama leo nchi hii ikaamua kwamba hawa wanasiasa wachache “mafisadi wa kufikirika” watoswe baharini au wafungwe maisha, je, CCM sasa itapona, au ndiyo itakuwa mwisho wa vitendo vya rushwa na ubadhirifu nchini mwetu? Mimi nasema hapana.

Mimi siwezi kumtetea mtu yeyote fisadi mradi ushahidi uanikwe wazi kwa kufuata mkondo wa sheria, lakini nisichokubaliana nacho ni kelele tu za ufisadi wa kufikirika na usiotolewa ushahidi thabiti kwenye vyombo vya sheria.

Nisichopenda ni tabia ya viongozi wa CCM kutofuata misingi ya chama ya kujadili mambo ya ndani ya chama na kukosoana kwenye vikao vya ndani ya chama. Sipendi wanandoa kugombana hadharani hadi kuvuana nguo na kuanza kufukuzana wakiwa uchi mitaani mbele ya watoto wao na watu wengine wa mitaani!

Kuhusu tuhuma zingine za kufikirika za “mafisadi” kupeleka fedha nyingi kwenye majimbo ya “wapambanaji wa ufisadi” ili kuwang’oa ubunge, nilisema kama ushahidi hauwezi kutolewa kuonyesha nani katoa fedha, kampa nani, lini, na zimepelekwaje kwenye majimbo hayo, basi shutuma hizi nazo ni za kufikirika, zisizokuwa na ukweli na ni woga tu wa hao wanaozitoa katika kujaribu kukandamiza demokrasia ya wagombea wengine kwenye majimbo hayo ili kupata huruma isiyostahili ya wapiga kura. Wengi kati ya hawa wanaopiga kelele hizo waliingia Bungeni mwaka 2005 baada ya kuwatoa wabunge waliokuwepo.

Je, wao “wapambanaji” walitumwa na mafisadi gani wakati huo ili kuwatoa waliokuwepo? Kama wameshindwa kuwashawishi wapiga kura wao kwa kutekeleza na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuondoa kero za wananchi wao, wasitafute wachawi.

Ni lazima sasa chama kisimame imara, kiache tabia ya kuogopa kuambizana ukweli na kiwakemee watu hao wanaotaka kukigawa na kukisambaratisha chama chetu, na ikibidi kiwavue uanachama ili tubaki na wanachama wanaokipenda chama chao kikweli na wanaofuata miiko, taratibu na maadili ya chama.

Dr. Milton Makongoro Mahanga, Mb, MNEC

2 comments:

Anonymous said...

Mahanga hakuna unachokisema hapa, maana unakubali mara unakanusha unataka uelewekeje? uji kuwa usuruhishi wa ndoa unaposhindikana kufanyika ndani ya ndoa kinachofuata ni kelele kutoka nje ya nyumba?
Hivi baadhi ya kesi za ufisadi amabazo zipo mahakamani haziwahusu baadhi ya wana ccm waliokuwa vigogo ndani ya chama na serikali? wewe unathamini sana chama kuliko wananchi wanaoteketea ndio maana tetezi yako yote ipo katika kukihami chama.
waache wenye uchungu na nchi hii waseme ukweli wewe endelea kukaa kimya na kukikumbatia chama chako.

Anonymous said...

tuelewe lipi mbona unajikanyanga? na iwapi chuki kisiasa dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi? Au nawe ni mmoja wao? Kwa nini uingize masuala ya chuki binafsi? Ina maana kamati zote za bunge zilizohusika na kuchunguza ufisadi zina chuki binafsi na watuhumiwa au wote waliotajwa kuwa wawajibike kwa nafasi zao kuhusiana ufisadi? Ama kwa hakika umefilisika kisiasa na kifikira. Inasikitisha. Sasa tutaanza kuhoji kuhusu udaktari wako iwapo unajikanyagakanyaga namna hii. Aibu tupu.

Post a Comment