Sunday, July 03, 2005

Mwamoto: Mwanasoka aliyehamia kwenye siasa

SPIKA wa Bunge, Pius Msekwa, awapo bungeni ni mtu wa utani sana. Yeye hupenda kumuita Mbunge wa Kilolo mkoani Iringa, Venance Mwamoto kwa utani ‘Mwafire’.

Kutokana na utani huo wa Spika, wabunge wengine wazoea jina hilo na wengi wao sasa wanamuita Mwafire na yeye hakatai, analipenda jina hilo.

Mwamoto (42), ni mbunge aliyeingia bungeni miaka mitano iliyopita, akiwa miongoni mwa wabunge vijana. Ni mbunge ambaye huwezi kumwelezea bila kuhusisha maisha yake na maendeleo ya soka la Tanzania.

Mbali na utalaam wake katika masuala ya uchumi, Mwamoto ametumia muda wake mwingi kucheza soka ndani na nje ya Tanzania.

Mbunge huyo aliyewahi kuwa mwanariadha, anasema hiviu karibuni alichaguliwa na umoja wa wacheza soka nchini kuwa Rais wao, katika chama chao kinachofahamika kama Soccer Players Union of Tanzania (SPUTANZA).

Mbali na chama hicho, mbunge hiyo aliyewahi kucheza katika timu ya Taifa ya vijana Timu ya Taifa (ya wakubwa), ni mjumbe wa Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Kipaji chake cha kucheza soka si tu cha kulazimisha, bali cha kuzaliwa kwani alianza kucheza tangu utotoni na aliwahi kuwa katika timu za Taifa za shule za msingi, umitashumta na umiseta kwa sekondari.

Mbali na michezo kuwemo damuni mwake, mbunge huyo aliisomea na kutunukiwa Diploma katika Physical Education, Sports and Culture.

Uzoefu, elimu na mazoezi vilimwezesha Mwamoto kuwika katika timu Kihesa Stars na Lipuli za Iringa, RTC Kagera, Majimaji ya Songea, Timu za Taifa na pia timu mbalimbali katika nchi za Sweden na Marekani.

Kwa vyovyote vile, Mwamoto ni moto wa kuotea mbali na ametoa mfano mzuri kuwa soka hata likiwa 'dogo' kama la Tanzania linaweza kukuinua. Amefuta mawazo ya wengi hapa Tanzania kuwa wacheza soka ni wahuni tu.

No comments:

Post a Comment