Monday, March 07, 2005

WAMEFIKA WANANE, RAIS HAJAPATIKANA!

It’s now official! Watanzania wanane wameingia katika mbio za kwenda IKULU. Kila mmoja kati yao, anasema, ‘mimi ndio nafaa’, binafsi, sijui nani kati yao anafaa kukalia kasri nyeupe peee, pale ufukweni mwa Bahari ya Hindi na mara chache sana, CHAMWINO, km 35 Mashariki mwa Mji wa Dodoma.

Wote wanataka kumrithi Rais Benjamin Mkapa. Kati ya waombaji hao wa uteuzi wa Chama Tawala, CCM, bila shaka kuna mwenye sifa zinazofaa kuteuliwa, au anaweza kujitokeza mwingine akabadili historia. Wote wameieleza sababu za wao kuingia katika mbio hizo, wengine wanadhani kupakana matope ni kampeni nzuri kwao, badala ya kujinadi kwa kutaja mazuri yao.

Kwa taratibu za CCM, kila mwombaji anatakiwa kutoa sh 1,000,000 ambazo hazitarejeshwa (non refundable). Kwa maana hiyo katika siku nne, tu, CCM imeingiza sh milioni 8 zisizolipiwa kodi. Mamlaka ya Mapato (TRA) mpo?

Waombaji wenyewe ndio wa CCM ni hawa; leo, nawazungumzia hawa tu, bila kugusia kambi ya upinzani, kwa sababu kwa hali ilivyo, yule atakayeteuliwa na CCM ndiye mwenye nafasi kubwa ya kushinda urais wa Tanzania katika Awamu ya Nne.

1. Waziri Mkuu, Frederick Sumaye
2. Makamu Mwenyekiti wa CCM, John Malecela
3. Waziri wa Mambo ya Nje, Jakaya Kikwete
4. Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Mark Mwandosya
5. Waziri, Ofisi ya Rais (Ubinafsishaji, Mipango), Dk.Abdallah Kigoda
6. Katibu Mkuu (Mstaafu) wa OAU, Dk. Salim Ahmed Salim
7. Mbunge wa Ilala, Iddi Simba; na
8. Balozi wa Tanzania, Ujerumani, Uswis na Poland, Ali Karume

Je, kati ya hao, mpenzi msomaji wa blogu, unaona rais ameshapatikana? Anaweza kuwemo kati yao, au akaja baadaye, kwani muda wa kuchukua fomu za CCM bado upo hadi Aprili 15, 2005. TUSUBIRI TUONE.


No comments:

Post a Comment