Monday, May 18, 2009

Kampeni za Busanda ni ‘jando ya kisiasa’

Uchambuzi huu kwa mara ya kwanza ulichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi Jumapili, Mei 17, 2009

Na Reginald Miruko

KWENDA jandoni ni msemo uliozoeleka katika makabila mengi nchini. Ni maneno mawili yanayoelezea dhana nzima ya watoto wa rika fulani—wanaohama kutoka utoto kwenda utu uzima, kwa lengo la kupewa mafunzo na nyenzo za kuwasaidia kuishi kama watu wazima. Ni wakati kuwafunza vijana waliopevuka jinsi ya kuendesha familia zao, kuishi na watu na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wao na jamii kwa ujumla.

Maelezo hayo mafupi yanatosha kufafanua maana ya sentensi hiyo— “Kwenda Jandoni”. Nimeamua kuutumia msemo huu katika uchambuzi huu ili kuonyesha uzito wa mafunzo yenyewe wanayoyapata wanasiasa wetu, vyama vyetu na Watanzania kwa ujumla kutokana na uchaguzi huo.

Kwa ufupi, uchaguzi huu wa Busanda una mafunzo yanayoweza kuzisaidia siasa za Tanzania zinazoendelea kukomaa taratibu. Kwa mtazamo wangu—ni uchaguzi mgumu kwa kila chama, iwe CCM iliyokuwa inashikilia jimbo, Chadema inayoshambuliwa kila upande, CUF iliyoshika nafasi ya pili mwaka 2005 na UDP.

Pamoja na maelezo ya CCM kuwa ina uhakika wa kulitwaa tena jimbo hilo kwa sababu lilikuwa lake na kuwa mwaka 2005 ililipata kwa asilimia zaidi ya 60, uhalisia ni kwamba, mambo bado magumu kwake na kulingana na taarifa zilizopo, inahitaji nguvu za ziada kulinyakuwa tena.

Hoja ya CCM na hali halisi jimboni inatoa funzo moja kubwa—kwamba hakuna jimbo la chama fulani milele na kwamba kura ambazo chama fulani kilipata katika uchaguzi uliotangulia si sababu wala kigezo cha kuendelea kulishinda, hasa kama matarajio ya waliokupigia kura hayajatimia.

Lolote linaweza kutokea baada ya uchaguzi wa Jumapili ijayo, lakini hadi sasa inaelezwa kuwa chama hicho kikongwe kimekabwa koo na wapinzani—hasa Chadema. Hoja kubwa ya kubanwa mbavu ni kwamba ahadi ya CCM ya kuwaletea umeme wakazi wa Busanda haijatimia na wananchi wengi wa eneo hilo wanaojishughulisha na uchimbaji mdogo madini, wamekata tamaa kwa maeneo yao kugawiwa kwa wawekezaji wa kigeni.

Yanayotokea katika kampeni hizo hadi sasa, ndio niliyoeleza hapo juu kuwa ni sawa na ‘jando ya kisiasa’—yanatufunza mambo mengi yatakayowazindua Watanzania usingizini wajue kwamba, hakuna chama chenye hakimiliki ya jimbo. Kinachotakiwa ni kwamba, baada ya kukiamini na kukichagua kinatakaiwa kutekeleza ahadi zake na kutatua matatizo yao.

Chama kinachofanikiwa kupata nafasi ya kuongoza kijue kuwa wananchi wa sasa wana elimu ya kutosha, wengi wamekwenda shule na wanafahamu kile wanachoahidiwa. Zaidi ya yote Watanzania bado wana matatizo mengi, kubwa likiwa la umaskini, hivyo aliyechaguliwa anatakiwa kushirikiana nao kuyatatua na juhudi zake binafsi na za chama chake zielezwe wazi na kuonekana badala ya kupiga tu propaganda.

Chama kinachoshinda uchaguzi kitambue kuwa zile zama za kugawiana khanga, fulani na takrima kisha kikachaguliwa kwa kishindo na kuondoka hadi uchaguzi mwingine, zimepitwa na wakati. Pia kwamba, mafunzo haya ya ‘jando ya kisiasa’ yanazidi kusambaa kwa wananchi na katika majimbo mengine, hivyo yanaweza kuwaathiri zaidi ‘waliozoea’ kukaa madarakani miaka mingi kama hawatabadilika.

Matukio ya kuzomeana kwenye kampeni za CCM na zile za UDP nayo yana mafunzo mengi ya ‘jando ya kisiasa’, yanayoonyesha si tu kwamba, wananchi wamechoka bali pia hawana namna nyingine ya kuonyesha kuchoka kwao zaidi ya kusema hadharani.

Hoja kwamba wazoemeaji wameandaliwa na Chadema inayotolewa na Viongozi wa CCM na wale wa UDP mimi naiona ni dhaifu kiasi fulani, kwani katika hali ya kawaida, siamini kama ni rahisi chama kufanikiwa kuwashawishi watu wengi kiasi hicho, wakaacha kampeni za mgombea wao wakawa na jukumu moja tu la kuifuata mkutano wa wapinzani wao kwa nia ya kuwazomea.

Pia si rahisi wazomeaji hao wa kulipwa wakachagua chama kipi cha kuzoea na kipi cha kuacha—maana hatujasikia wakiwazomewa CUF na mgombea wao. Hata wanafunzi wakalipwa ili wazomee chama ‘kinachokubalika’! Bila shaka ni wananchi wa kawaida, waliozibwa midomo muda mrefu, waliokata tamaa na hatimaye wakapata fursa ya kueleza hisia na matatizo yao.

Yanayomkuta Cheyo na chama chake cha UDP kwa sasa yanaweza kufananishwa na yale yaliyomkuta Mchungaji Christopher Mtikila na chama chake cha DP na kile cha NCCR-Mageuzi kwenye uchaguzi wa Tarime, kwa kudhaniwa kuwa ameingia kuisaidia CCM. Katika eneo hili pia kuna mafunzo ya ‘jando ya kisiasa’.

Jambo jingine ambalo linaweza kuwa funzo la ‘jando ya kisiasa’ kwetu ni kufahamu Chadema ilikopata nguvu za kuwasumbua wanasiasa wengine, wakiwamo wakongwe wa siasa na matingatinga ya chaguzi ndogo. Hili liko wazi, Chadema walijiandaa mapema, walifanya kile ambacho vyama vingine vimeshindwa. Waliandaa mapema ‘Operesheni Sangara’ ya kuhamasisha wananchi katika mikoa mbalimbali. Geita lilipo Jimbo la Busanda nako walipita na kumwaga sumu yao.

Nimeelezwa kuwa hata Biharamulo Magharibi unapotarajiwa kufanyika Uchaguzi Mdogo Julai 5, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameshafanya mkutano wake mkubwa siku chache baada ya kushiriki mazishi ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Phares Kabuye. Na hilo ni Jando la kisiasa linalopaswa kuigwa na vyama vingine ambavyo havina mzizi katika maeneo ya vijijini.

Mbali na kupitapita kwa wananachi katika ‘Operesheni Sangara,’ wabunge wa chama hicho wakiwa watano wa kuchaguliwa na sita wa viti maalum wameonyesha wanachokifanya bungeni. Wananchi wameanza kuwaamini. Wanawaunga mkono. Hilo pia ni funzo na jando la kisiasa kwa vyama na wabunge wengine.

Simu 0713 346175






No comments:

Post a Comment