Monday, April 11, 2011

Nyoka akivua gamba anakuwa nani?Nijuavyo mimi nyoka akijivua gamba hawezi kuwa kenge. Atabaki ni nyoka. Kama ni kifutu atakuwa vile vile, kama ni swila atakuwa vivyo hivyo, n.k

Ok, CCM imejivua gamba kama wanavyotamka wenyewe, kwa hiyo watakuwa tofauti na walivyokuwa awali? Wale waliopandikizwa na mafisadi katika chaguzi mbalimbali kuanzia kata, wilaya, mikoa, wajumbe wa NEC
watakuwaje? Au nao watoswe ili iwe ile hadithi ya kujivua ngozi nzima badala ya gamba?

Sawa, hawa wachache wa Kamati Kuu na Sekretarieti wametoswa, lakini kwa nini gamba halikuvuliwa kuanzia kichwani, badala yake likaanzia mabegani hadi miguuni? Kwa nini kichwa kibaki na gamba lile lile lililochuja, halikubaliki kwa wanachama na wananchi kwa ujumla? Au hikii ni kichwa na mnyama mwingine tofauti na nyoka?

Kuna jamaa mmoja kwenye mijadala ya mitandaoni, amehoji: Hivi kuchoma kichaka ili kuharibu miti michache minovu ni busara? Au busara ilikuwa ni kuchambua miti mibovu na kuacha mizuri na kichaka kikaendelea kushamiri. Kwa maoni yake, kasoro iko kwa kiongozi aliyeshindwa kuchagua miti mibovu ili kubakiza mizuri, badala yake akachoma kichaka kizima ili kuepuka lawama.

No comments:

Post a Comment