Friday, March 19, 2010

JK ampongeza Balozi wa Papa Mtanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo, Alhamisi, Machi 18, 2010, ametuma salamu za pongezi kwa Monsinyori Novatus Rugambwa (pichani), Mtanzania, ambaye ameteuliwa na Papa Benedict wa 16 kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki na Balozi wa Papa katika nchi mbili za Afrika za Angola, na Sao Tome na Principe.

Monsinyori Rugambwa amesimikwa kushika daraja la uaskofu mchana wa leo na Mwadhama Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu Mkuu wa Nchi wa Baba Mtakatifu, katika Misa maalumu ya kuwekewa wakfu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, Vatican.

“Baba Askofu, nimepokea kwa furaha nyingi na faraja kubwa habari za uteuzi wako wa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki na Balozi wa Papa katika nchi za Angola, na Sao Tome na Principe,” Mheshimiwa Rais Kikwete amesema katika salamu hizo za pongezi na kuongeza:

“Kwa niaba ya Watanzania wenzako, kwa niaba ya Serikali yangu na kwa niaba yangu binafsi, napenda kukupongeza sana kwa uteuzi huo. Uteuzi huo ni heshima kwa nchi yako, ni heshima kwa Watanzania wenzako na ni matokeo ya utumishi wako uliotukuka katika Kanisa. Ni nafasi unayoistahili.”

Amesisitiza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Napenda kuchukua nafasi hii kukutakia kila la heri katika utumishi wako kwenye nafasi hizi mpya. Aidha, napenda kukuhakikishia kuwa Watanzania wenzako na mimi tutaendelea kukuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe nguvu na afya njema ili uweze kumudu nafasi hizo.”

Monsinyori Rugambwa mwenye umri wa miaka 52 anakuwa Mtanzania wa kwanza kuteuliwa kuwa Balozi wa Papa.

Kabla ya uteuzi wake, Monsinyori Rugambwa alikuwa Msaidizi wa Katibu katika Baraza la Wakimbizi la Serikali ya Vatican – Ponticifal Council for the Pastoral Care of Mingrant and Itinerant People, nafasi aliyoishikilia tokea Juni 28, 2007.

Kabla ya hapo alikuwa mshauri wa Balozi wa Papa nchini Indonesia. Awali alikuwa mtumishi wa Balozi za Papa katika Panama, Jamhuri ya Congo, Pakistan na New Zealand.

Alijiunga na Utumishi wa Nchi za Nje wa Serikali ya Vatican mwaka 1999. Ana Shahada ya Uzamivu ya Sheria za Kanisa na anazungumza vizuri lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kihispanishi na Kijerumani. Alipata daraja la upadre mwaka 1986.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
18 Machi, 2010

No comments:

Post a Comment