Monday, February 09, 2009

Zombe ana kesi ya kujibu

Watatu waachiwa huru

Washtakiwa watatu katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdalah Zombe na wenzake 12 wameachiwa huru mchana huu baaada ya kuonekana hawana kesi ya kujibu.


Washtakiwa hao ambao waliondoka mahakama kuu wakiwa watu huru ni mshtakiwa namba 4, namba 6 na namba 8. Washtakiwa hao ni Noel Leonard, Moris Nyangelela na Felix Cedrick.


Kesi imeahirishwa hadi kesho ambapo washtakiwa wataanza utetezi baada ya kula kiapo kilichoshindikana kuliwa leo. Akitoka mahakamani na kupanda karandinga, Zombe alisikika akisema mambo yote kesho na kwamba nchi inaendeshwa kwa utawala wa sheria.


Wiki iliyopita, mawakili wa pande zote walijenga hoja kuishawishi mahakama kukubaliana na maoni yao, baada ya upande wa mashitaka kumaliza kutoa ushahidi wao.


Wakati upande wa mashitaka unasisitiza kuwa Zombe na wenzake wana kesi ya kujibu, upande wa utetezi unadai hakuna ushahidi mzito unaowafanya
washitakiwa hao wasimame kizimbani kujitetea.


Zombe na wenzake wanashitakiwa kwa mauaji ya Wafanyabiashara wanne ambao ni Ephrahim Chigumbi, Sabinus Chigumbi ‘Jongo’, Mathias Lunkombe na Juma Ndugu, ambaye alikuwa dereva wa teksi iliyokuwa ikitumiwa na wafanyabiashara hao katika shughuli zao.


Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 26/2006 ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makele, F. 5912 Konstebo Noel Leonard, WP. 4593 Konstebo Jane Andrew, D. 6440 Koplo Nyangelera Moris na D. 1406 Koplo Emmanuel Mabula.


Wengine ni E. 6712 Koplo Felic Sandsy Cedrick, D. 8289 Konstebo Michael Shonza, D. 2300 Koplo Abeneth Saro, D 9321 D/C. Rashid Lema, D. 4656 D/Koplo Rajab Bakari na D. 1367 D/Koplo Festus Gwabisabi.

No comments:

Post a Comment