Friday, February 13, 2009

KICHAPO CHA WALIMU, WAZIRI AJA JUU

Kichapo


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantum Mahiza amelaani kitendo cha Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Kanali Albert Mnali kuwacharaza walimu bakora kwa sababu ya shule zao kufanya vibaya katika mitihani ya taifa na wilaya yao kuwa ya mwisho.


Mahiza alisema jana kuwa haiingii akilini kama DC anaweza kufanya kitendo hicho, hivyo akapendekeza apimwe akili kuona kama yuko sawasawa.

Wakati Mahiza akisema hayo, bosi wake, Profesa Jumanne Magembe alisema kwamba kamwe hawawezi kulivumilia. "Ni kweli kuna tukio la aina hiyo na nimeshamwagiza mkuu wa mkoa kufanya uchunguzi na endapo ukweli utapatikana, serikali itachukuwa hatua kali dhidi ya wahusika," alisema Profesa Magembe na kuongeza:

"Nchi yetu haiwezi kuongozwa na watu wa aina hiyo na kamwe serikali haiwezi kukaa kimya... mara tu baada ya mkuu wa mkoa kumaliza kazi yake, atatuletea taarifa na sisi tutalifikisha kwa waziri mkuu kwa hatua zaidi kwani hao wote wako chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu". "Hilo ni tukio
la aina yake na la kusikitisha sana kwa sababu binadamu hawezi kuongozwa njia kwa kuswagwa kama ng'ombe... ni lazima serkali ichukue hatua kali dhidi ya wahusika".

Kwa uapnde wake, Rais wa CWT, Gratian Mukoba alisema suala hilo si jepesi na kwamba mkuu huyo wa wilaya ametonesa kidonda kibichi kwa kukitia chumvi hivyo aliyemweka serikalini mkuu huyo ndio
atakayemtoa na kumchukulia hatua.

Alisema taarifa hiyo waliipata saa 5:00 asubuhi juzi ofisi yake walipokea barua pepe kutoka katika chama cha walimu, tawi la Kagera iliyoeleza kuwa mkuu wa wilaya anatembelea shule za msingi wilayani kwake na kutoa adhabu ya viboko kwa walimu.

No comments:

Post a Comment