Thursday, November 25, 2004

Uchambuzi wa Mwaka

Staili ya CPC kulinda maadili ya Uandishi wa Habari ina kasoro

Na Reginald Simon, Dodoma

MEI 18 Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Waandishi wa
Habari wa Kanda ya Kati (CPC), yenye makao yake makuu
mjini hapa, ilitoa ‘hukumu’ ya kihistoria kwa nia ya
kurejesha maadili ya uandishi wa habari yaliyopotea.

Katika hukumu hiyo iliyomo kwenye taarifa ya Katibu
Mkuu wa CPC, Lucas Lukumbo kwa vyombo vya habari,
mwandishi wa kujitegemea, Kulthum Mchata, anayeandikia
Radio Free Africa (RFA) na Televisheni ya Star,
alipata adhabu kali, ambayo haijawahi kutolewa na
klabu yoyote ya waandishi wa habari nchini.

Ni adhabu kali kwa sababu pamoja na kwamba binti huyo
hajawahi kuonywa kwa kosa lolote, amesimamishwa
uanachama wa CPC kwa miezi mitatu na kuzuiwa kufanya
kazi ya uandishi wa habari mkoani Dodoma kwa muda huo
huo.

Kinachogomba hapa si kumsimamisha Kulthum uanachama wa
CPC kwa kukiuka maadili ya uandishi wa habari, bali
kuzuiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari mkoani
Dodoma kwa miezi mitatu. Hili linagomba kwa sababu CPC
haina kanuni wala kipengele cha katiba kinachoipa
mamlaka hayo. Imejipachika madaraka.

Kamati ya Utendaji ya CPC, kwa mujibu wa katiba yake,
chini ya kifungu cha 4:3.5.2 inatakiwa kuhakikisha
kwamba wanachama wa CPC wanakuwa na nidhamu na kufuata
maadili ya uandishi wa habari.

Pia, kifungu cha 4: 3.5.6 kinaipa mamlaka kamati hiyo
kumsimamisha uanachama, mtu yeyote atakayekiuka
maadili ya uandishi wa habari.

Ieleweke kuwa hakuna kifungu chochote ndani ya katiba
hiyo kinachoipa kamati hiyo wala mkutano mkuu wa CPC,
mamlaka ya kumsimamisha mwanachama kufanya kazi ya
uandishi wa habari wala kumfukuza kazi hiyo.

Kwa uelewa wangu ‘hukumu’ hii itakuwa ya kwanza ya
aina yake katika historia ya taaluma ya uandishi wa
habari nchini, kwani sijawahi kusikia klabu yoyote
ikitoa uamuzi kama huo.

Vile vile, si Baraza la Habari ambalo ni mlezi wa
vilabu hivyo na msimamizi wa maadili hayo wala Idara
ya Habari (MAELEZO), wala Bunge la Jamhuri lililowahi
kulalamikiwa kwa kuwaita na kuwahoji baadhi ya
waandishi na wahariri, lililowahi kutoa uamuzi wa aina
hiyo.

Uamuzi wa aina hiyo haujawahi kutolewa na asasi hizo
za habari, licha ya kuwepo malalamiko mengi ya
waandishi wa habari makanjanja, wanaoidhalilisha
taaluma hiyo. Inawezekana asasi hizo hazijatoa maamuzi
ya aina hiyo kwa sababu hazina mamlaka hayo ambayo CPC
imejipachika.

Si nia yangu kutetea makosa ya ukiukaji wa maadili ya
taaluma ya uandishi wa habari. Hakuna siri tena kwa
taaluma ya uandishi wa habari mkoani Dodoma na maeneo
mengine ya Tanzania imekuwa ikidhalilishwa kwa muda
mrefu na zinahitajika mbinu mbalimbali kuirejeshea
heshima yake.

Binafsi, naungana na mbinu mbalimbali za kuirejeshea
taaluma ya uandishi wa habari heshima yake, na
waandishi wanaoonekana kama makanjanja ‘wachovu’
waheshimiwa tena kama ilivyokuwa zamani, lakini
sitaunga mkono mbinu chafu, zinazokiuka katiba, sheria
na taratibu walizojiwekea wanataaluma wenyewe kwa
kivuli cha kulinda heshima ya taaluma ya uandishi wa
habari.

Labda, msomaji nikurejeshe katika tukio lilimkuta
Kulthum hadi akakumbana na adhabu kubwa namna hiyo ya
kumsimamisha kazi kabla hata ya mwajiri aliyempa kazi
hiyo kutoa kauli yoyote juu yake.

Inasemekana, binti huyo alimshtaki Afisa Habari wa
Maelezo mkoani hapa, Jamal Zuberi kwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Alhaji Musa Nkhangaa kwa kutoandika jina lake,
katika orodha ya waandishi wa habari waliotakiwa
kulipwa posho kwa kuandika habari za Siku ya Malaria
Afrika, Aprili 25, mwaka huu, katika uwanja wa Jamhuri
mjini hapa.

Imedaiwa kuwa, vile vile kuwa mwandishi huyo
amelalamikiwa na Baraza la Waandishi wa Vitabu
Tanzania (UWAVITA) kuwa amechukua posho ya mkutano
ambao hakuhudhuria.

Kwa maoni ya Kamati ya Utendaji, matukio hayo ni
ukiukaji wa maadili ya uandishi wa habari, lakini
mazingira ya tukio zima yanatia shaka kwa sababu
katika kamati mbili zilizofikia uamuzi huo, ile ya
maadili na ya utendaji wamo watu wanaoonekana hawawezi
kumtendea haki mlalamikiwa.

Mbali na kuwepo mlalamikaji, Zuberi, pia kuna mjumbe
mmoja ambaye amekuwa anagombana na mlalamikiwa mara
kwa mara, kwa kinachodaiwa kuwa ni maslahi ya kikazi.

Yapo madai kutoka kwa waliohudhuria mkutano wa
UWAVITA, kuwa afisa mmoja wa CPC ambaye hawaelewani
siku nyingi na Kulthum, ndiye alimlalamikia mwandishi
huyo kuwa amechukua posho bila kuwepo, na
‘kuwalazimisha’ wahusika kumlalamikia kwa maandishi.

Ni jambo la kushangaza pia kuwa, wajumbe wa Kamati ya
Utendaji ya CPC waliofikia maamuzi hayo na kuandika
taarifa kwa vyombo vya habari, ndio wamekuwa wa kwanza
kuandika habari za mwandishi huyo kwenye vyombo vya
habari wanavyowakilisha. Huo pia ni ukiukaji mkubwa wa
maadili ya uandishi katika kipengele cha Mgongano wa
Maslahi (Conflict of Interest)

Pamoja na waandishi wengi wa habari wanaounda CPC
kutoafikiana na vitendo vya ukiukaji wa maadili,
hawaungi mkono hatua zilizochukuliwa dhidi ya binti
huyo. Wanasema ni uamuzi wa hasira, na Kulthum
ametolewa kafara.

Taarifa ya CPC haikuishia tu kutoa adabu kwa mwandishi
huyo, bali imevishauri vyombo vyote vya habari nchini,
kutomtumia mwandishi huyo katika kipindi chote cha
adhabu yake, ili kumpa nafasi kujirekebisha na wakati
huo huo, iwe funzo kwa waandishi wengine wanaojihussha
na vitendo kama hivyo.

Nionavyo mimi, Kulthum Mchatta ameonewa. Anastahili
kudai haki yake kwa kukata rufaa ndani ya chama
chenyewe, au kwenda mahakamani kupinga adhabu hiyo.

Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kwani CPC ina
madaraka ya mwisho kama alivyo Mungu. Haina kipengele
cha rufaa katika katiba yake wala hakuna kanuni
inayoelezea namna ya kufanya hivyo.

Pamoja na kuwepo uwezekano kuwa mwandishi huyo
ametenda kosa kitaaluma, ni vizuri mwajiri wa Kulthum
akachukulia uamuzi huo wa CPC kwa makini, akafanya
uchunguzi, ili asije akajikuta anaunga mkono maamuzi
yaliyochukuliwa kwa jazba bila kuzingatia katiba ya
klabu.

Vile vile ninaushauri uongozi wa CPC ambao ni mpya
madarakani, ufanye kazi zake kwa kuzingatia Katiba.
Kama wanaona katiba hiyo ina mapungufu, waandae
mazingira ili ifanyiwe marekebisho kuliko kuchukua
maamuzi ya ajabu ambayo hayajawahi kutokea nchini.

Ninasikia pia uongozi huo umeteua wadhamini wapya
kisirisiri na kuwatumia barua za uteuzi bila hata
kuleta hoja hiyo katika mkutano mkuu wa CPC kama
inavyotakiwa.

Endapo maamuzi ya namna hiyo yataendelea kutolewa kwa
kufunika macho yao kwa blanketi zito ili wasione
sheria, CPC itavurugika tena, kama ilivyokuwa katika
kwa awamu iliyoisha.

Uongozi wowote ili uwe halali lazima uzingatie sheria
na katiba iliyouweka madarakani. Kwa maneno mengine
lazima uzingatie utawala wa sheria, vinginevyo
hautaheshimkika wala kukubalika kwa wengi.


Reginald Simon, ni mwanachama wa CPC na mwakilishi wa
gazeti la Mwananchi mkoani Dodoma. Simu 0741 346175 e-mail:
rsmiruko@yahoo.co.uk, website: www.rsmiruko.blogspot.com

mwisho


4 comments:

Anonymous said...

hii ya kulthum hata kama ni ya siku nyingi mzee nakupa Big up kwa kueleza bayana uhalisia wa jambo lenyewe. Hongera sana

Anonymous said...

Mzee RSM, naomba kwanza utupe CV za viongozi hao wa CPC ili tujue hali yao Kitaaluma, maana hapo naona kuan mambo mengi sana kuanzia conflict of interest, professionalism na hata press freedom.Ntaka nijue hayo ya CV maana pengine CPC ni chombo ambacho kimejaa watu wanaopinga kitu kinachoitwa Freedom of speech, Press Freedom,ethical journalism na keeeping the right of the people to be informed.Sitosema chochote mpaka mzee RSM unipatie hayo maana hii issue ni kati yenu waaandishi ambao huwa mnalalamika sana juu ya uhuru wa vyombo vya habari.

Anonymous said...

Mzee RSM, naomba kwanza utupe CV za viongozi hao wa CPC ili tujue hali yao Kitaaluma, maana hapo naona kuan mambo mengi sana kuanzia conflict of interest, professionalism na hata press freedom.Ntaka nijue hayo ya CV maana pengine CPC ni chombo ambacho kimejaa watu wanaopinga kitu kinachoitwa Freedom of speech, Press Freedom,ethical journalism na keeeping the right of the people to be informed.Sitosema chochote mpaka mzee RSM unipatie hayo maana hii issue ni kati yenu waaandishi ambao huwa mnalalamika sana juu ya uhuru wa vyombo vya habari.

Anonymous said...

nashukuru sana kwa taarifa zenu, lakini shida yangu kuu, naomba unielekeze makao makuu ya uwavita

Post a Comment