Thursday, November 25, 2004

Tulipofikia kutoka Bungeni

Serikali imewekwa mfukoni?

Na Reginald Simon, Dodoma

SERIKALI imeshauriwa ama kukifunga au kukihamisha
kiwanda cha nguo cha Karibu (KTM) cha Mbagala, Dare s
Salaam ili kuwanusuru majirani dhidi ya athali za
uchafuzi wa mazingira.

Pamoja na ushauri huo, mbunge wa Kigamboni, Frank
Magoba (CUF) amelieleza bunge jana kuwa, ‘wananchi wa
Mbagala wana wasiwasi kuwa Jeta (mmiliki wa kiwanda
hicho) ameiweka serikali mfukoni’.

Mbunge huyo alikuwa akichangia Muswada wa Sheria ya
Mazingira wa mwaka 2004, uliowasilishwa juzi jioni na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na
Muungano), Arcado Ntagazwa na jana kupitishwa na
bunge.

Magoba alisema viongozi wengi, akiwemo Makamu wa Rais
wa zamani, marehemu Omar Ali Juma wamewahi kutembelea
KTM, lakini hakuna kinachofanyika kwa miaka kati ya
mitano na kumi, jambo ambalo linawatia wasiwasi.

Inaonekana kiwanda hicho kinaachiwa kwa sababu
kinalipa kodi, kodi isiwe sababu ya kuharibu maisha ya
watu,” alisema Mbunge huyo na kuhitmisha kuwa
asingeunga mkono sheria hiyo hadi apate maelezo.

Alisema endapo serikali haitakifunga wala kukihamisha
kiwanda hicho, basi mmiliki wake agharamie fidia ili
wananchi wanaoishi karibu nacho na kuathirika
wahamishwe.

“Watoto wadogo wanachezea maji machafu yenye kemikali
yanayotoka katika kiwanda hicho, wananchi wa pale
wanakohoa ovyo kutokana na moshi wa kiwanda hicho,”
alisema mbunge huyo.

Magoba alisema ataandika barua kwa Rais Benjamin Mkapa
na nakala kmpatia waziri anayehusika na Mazingira
kulalamikia kiwanda hicho ili hatua za haraka ziweze
kuchukuliwa.

Vile vile Mbunge huyo alimshauri mmiliki wa kiwanda
hicho alichodai kimekuwa kinabomoka bomoka kutokana na
ujenzi usio wa kitaalam, atumie gesi ya songosongo ili
kuondoa tatizo moshi.

Akijibu hoja za mbunge huyo, Ntagazwa alisema serikali
haiwezi kuthamini sana kdi kuliko masha ya wananchi
wake na imekuwa ikichukua hatua dhidi ya viwanda
vinavyochafua mazingira kikiwemo cha KTM.

Alisema aliwahi kutembelea kiwanda hicho akiwa na
watalaa wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
(NEMC) na kutoa maelekezo ya kufuata, ikiwa ni pamoja
na kusomesha wafanyakazi juu ya uzalishaji bora.

Mojawapo ha hatua zilizochukuliwa, Ntagazwa alisema,
ni kuleta muswada huo bungeni ili kuweka misingi
mizuri ya udhibiti, na kuipa NEMC ‘meno ya msumeno wa
umeme’ ili kuiwezesha kuwachukulia hatua wote
wanaochafua mazingira.

Muswada huo umependekeza kifungo jela hadi miaka 12 au
kulipa faini faini kati ya sh 50,000 na sh milioni 50
kwa wanakaovunja sheria hiyo.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mafia, Abdulkarim
Shaha ametishia kumfikisha katika Kamati ya Haki,
Kinga na Maadili ya Bunge Msemaji wa Kambi ya Upinzani
katika masuala ya Mazingira, Ali Said Juma (Kojani)
kwa madai ya kuwadhalilisha wakazi wa Mafia kuwa
‘hawana vyoo bali wanajisaidia ufukweni’.

Katika mchango wake, Juma alisema faini ya sh 50,000
inayotozwa kwa anayechafua mazingira, ni kubwa
itakayowashinda wengi hasa wakazi wa Ukerewe, Mwanza
na Mafia, Pwani ambao hujisaidia ufukweni, na itafika
hatua kijiji kizima kitaishia gerezani.

mwisho

No comments:

Post a Comment