Thursday, November 25, 2004

Yaliyojiri Dodoma Wiki Hii

Nov 24

Diwani atuhumiwa kwa mauaji

Na Reginald Simon, Dodoma

WATU 24 akiwemo diwani wakamatwa na polisi kwa tuhuma
za kumuua Mwenyekiti wa Kijiji cha Pwaga,John Msigala
(78) na mwanaye Silvano John (25).

Diwani huyo wa Kata ya Pwaga wilayani Mpwapwa,Acrey
Myang’ari,na wenzake 23 wanasubiri kupimwa akili
katika hospitali ya Mirembe kabla ya kufikishwa
mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.

Tayari gwaride la utambulisho limefanyika na baadhi
yao wametambuliwa lakini polisi mkoani hapa hawakutaka
kuelezea zaidi juu ya utambuzi huo.

Polisi Dodoma ilipeleka magari matatu, mawili kutoka
mkoani na moja wilayani Mpwapwa yenye askari katika
operesheni hiyo iliyoanza jioni hadi alfajiri saa 11
na kufanikisha kukamatwa kwa watu hao.

Wengine waliokamatwa katika operesheni ya polisi
iliyoendeshwa usiku mzima wa Novemba 17 kuamkia 18,
mwaka huu, ni Henry Mfugale, Yese Mponzi, Yusto Mahia,
Philipo Kinonge, Edward Msanda na Benson Chalo.

Wengine ni Stephen Mbwani, Peter Gwivaha, Bonface
Chawene, Damian Mkakala, Majuto Madani, Dickson
Mwigune, Ibrahim Mgewe, Alan Ngowo, Frederick Peter na
Sikujua Makasi.

Watuhumiwa wengine ni pamoja na Mathias Msumari, David
katamwa, Benson Mahogo, Mussa Kishumu, Sudi Mbaile na
Emmanuel Katamwa.

Kamanda wa polisi Mkoani Dodoma, Wolfugang Gumbu,
alisema hapa jana kuwa watuhumiwa hao ni kati ya
wengine zaidi ya 40 wanaosakwa na polisi kwa tuhuma za
mauaji hayo na kujeruhi watu wengine wanne wa familia
hiyo.

Polisi walipokea taarifa za mauaji hayo Novemba 9 kuwa
watu zaidi ya 80 walivamia familia hiyo na kuwaua
Msigala na mwanaye kwa madai kuwa mzee huyo anaishi
katika chanzo cha maji.

Baada ya kumuua mzee huyo kwa mapanga, wauaji
waliuchoma moto mwili wake na kuanza kuharibu mali
zake kadhaa na kuiba vitu mbalimbali yakiwemo mabati,
nguruwe na mbuzi

Kabla ya mauaji mzee huyo alipelekewa barua na
serikali ya kijiji kumtaka ahame katika eneo hilo kwa
madai kuwa ni chanzo cha maji, lakini mzee huyo
alikataa akisema eneo hilo liko kilometa moja kutoka
chanzo cha maji.

Polisi walijitetea kwa kushindwa kutoa taarifa hizo
kwa umma hadi watoto wa marehemu walipoamua kutangaza
habari hizo, kwa madai kuwa ‘ilikuwa mbinu yao ya
kukamata watu wengi zaidi waliohusika’.

"Watuhumiwa walikuwa wengi, kama tungekwenda bila
mpangilio wangeweza kutoroka wengi zaidi," alisema
Gumbu.

mwisho





No comments:

Post a Comment