Tuesday, February 17, 2009

Masha aingia rasmi vitani

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha jana alivunja ukimya wake dhidi ya tuhuma zinazomwandama kuwa aliingilia mchakato wa zabuni ya mradi wa uchapishaji vitambulisho vya taifa, alipokanusha kuwa na uhusiano wowote na kampuni ya Sagem Securite na kusema kuwa yuko tayari kujiuzulu iwapo itathibitika kuwa alifanya kosa hilo au alipokea rushwa.


Waziri Masha pia alisema kuwa taarifa za vyombo vya habari kuwa alikuwa nchini Uswisi Oktoba mosi kuzungumzia tenda hiyo, si sahihi na kuonyesha nyaraka za kusafiria zinazoeleza kuwa siku hiyo alikuwa akitokea Hong Kong kuja Tanzania.


Masha ameibuka kuzungumzia tuhuma zake siku moja baada ya Bodi ya Zabuni ya Wizara ya Mambo ya Ndani kutaja kampuni sita zilizopita ngwe ya kwanza ya mradi huo uliotengezewa zaidi ya Sh200 bilioni, huku Sagem Securite ikiwa imetupwa nje ya mchakato.



Kampuni zilizovuka hatua ya awali ya mchujo ni Unisys ya Afrika Kusini, Giesecke& Devrient Fze ya Dubai na Iris Corporation Berhad ya Malysia.



Nyingine ni Madras Security Printers ya India, Maruben Corporation ikishirikiana na Zetes na Nec ya Japan na Tata Consultancy Services ikishirikiana na na Ontrack Innovatives Limited ya India.



Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano maalumu na wahariri na wawakilishi wa wahariri wa vyombo vya habari, Masha alisema ameamua kuvunja ukimya baada ya kuona mchakato huo sasa unazungumzika hadharani na kwamba yuko tayari kujiuzulu kama kuna uthibitisho wa yeye kuingilia zabuni.



Masha, ambaye alionekana kutokuwa na wasiwasi, alichambua tuhuma moja baada ya nyingine na kusema hajawahi kuwa na ukaribu na Sagem Securite ya Hispania zaidi ya kupokea malalamiko yao na kuongeza kwamba uamuzi wa kutaka ushauri wa Mamlaka ya Umma (PPRA), wakati mchakato ukiendelea, haukuingilia mchakato.



Kuhusu kilichoitupa nje Sagem Securite katika hatua ya awali ya mchakato, Masha alisema hiyo haikutokana na kukosa sifa au uwezo, bali ni kuvuja kwa taarifa kutokana na nyaraka iliyonyofolewa hivyo kuathiri taratibu za kisheria za zabuni ambazo ni siri.

No comments:

Post a Comment