Mazungumzo ya mwisho na Mzee Phares Kabuye
Na Reginald Miruko
Juzi nilitoka Biharamulo, mkoani Kagera, kwenye mapumziko yangu. Siku naelekea huko, kwenye basi la Nyehunge mjini Mwanza, nilimuona Mzee Phares Kabuye.
Huyu ni mbunge wa zamani wa Biharamulo Magharibi, aliyewahi kuongoza jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo katika miaka ya 90 na baadaye kuondolewa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwa amemaliza miezi 20 ya kipindi cha tatu.
Kama mwandishi wa habari, wazo lilinijia kwamba nikifika jimboni kwake, nifanye naye mazungumzo juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo ya jimbo, rufaa yake katika Mahakama ya Rufaa ambayo haisikiki kwa muda mrefu, hali ya kisiasa wilayani kwake na mambo mengine. Hilo halikuwa taabu, kwani tulikuwa kwenye safari moja ya saa kama sita hadi mjini Biharamulo.
Tulipofika Sengerema na basi kusimama, nilipata wasaa wa kuwasiliana naye, na kuomba miadi ya mazungumzo. Kama ilivyo kawaida yake, hakushanga, alikubali. Akanipa namba yake ya simu na mimi nikampa yangu, tukakubaliana kukutana baada ya Sikukuu ya Pasaka.
Siku mbili baada ya Pasaka, nilimpigia simu nikamkumbusha miadi yetu, na kuomba kuonana naye siku hiyo. Alikubali moja kwa moja, akanielekeza kwake.
“Njoo, niko nyumbani kwangu, ni karibu na mnara wa Celtel (Zein),” alisema kwa sauti yake ya juu, iliyokuwa imezoeleka kulitikisa Bunge. Nilitafuta usafiri wa pikipiki ambao ni rahisi na unaopatikana kwa wakati wote mjini Biharamulo. Haikunichukua dakika tano kutoka eneo la Umoja nilipokuwa, hadi nyumbani kwake.
Kinyume na matarajio yangu, ghafla niliona kijana aliyenipeleka anasimamisha pikipiki. Akasema ni hapa tumeshafika. Nikamuuliza, nyumba ipi? Kijana huyo akajibu hii hapa. Nilijitahidi nisishangae sana, niliteremka, nikamlipa Sh500 za usafiri na kuelekea kwenye nyumba niliyoelekezwa.
Mbele ya nyumba hiyo walikuwapo wanawake wawili waliokuwa wakiaanika mahindi. Niliwauliza kama mzee Kabuye nimemkuta. “Yule palee, anayefukuza mbuzi,” alisema mwanamke mmojawapo.
Nilimfuata alipokuwa, nyumba kama ya tatu, tukarejea wote hadi ndani kwake. Tulikaa kwenye makochi na kabla ya kuanza mazungumzo, kama kawaida ya mwandishi yeyote nilitupa jicho hapa na pale sebuleni kwale.
Niliona magunia kadhaa ya mahindi ambayo baadaye alikuja kukiri kuwa ni mazao yake ya kilimo, kazi ambayo hadi kifo chake alikuwa akiifanya. Ukutani kulikuwa na picha kadhaa, mojawapo amepiga na Waziri wa Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo John Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Biharamulo Masharikii na nyingine akiwa anasalimiana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Katika mazungumzoa yetu, Mzee Kabuye alisema matumaini yake ameyaweka kwenye Mahakama ya Rufani, akiamini kuwa kama watenda haki, atapata haki yake na kuepuka kulipa mamilioni ya fedha za fidia endapo atakubaliana na maamuzi ya Mahakama Kuu iliyotengua ubunge wake.
“Hayo mamilioni ya kulipa mimi sina. Nitakachofanya ni kusubiri kesi ifike mwisho, ninaamini nitapata haki yangu,” alisema Kabuye aliyekuwa na umri wa miaka 71.
Alisema endapo kesi yake itafikia mwisho na nafasi ya ubunge kutangazwa au ikichelewa hadi uchaguzi mkuu mwakani, atagombea tena nafasi hiyo.
Hakuona kama umri wake umekwenda? Akijibu swali hilo, alisema: “Ubunge ni wa wananchi. Ikifika uchaguzi watu wengi wanajitokeza, wamo vijana, wako wazee, wako wanawake, wananchi wanachagua wanayemtaka. Tukibaguana huyu mzee, kesho tutasema huyu mwanamke, kesho huyu kabila sio kabila letu. Huko bungeni hatuendi kukimbia wala kupigana ngumi, ni hekima na busara.
“Wananchi wanakwambia shida zao na nyingine unaziona mwenyewe, unazipeleka bungeni. Basi. Na Wananchi wa Biharamulo hawachagui chama wanachagua mtu,” alisisitiza Kabuye ambaye pia alikuwa mbunge wa Bunge la Afrika.
Akizungumzia matatizo ya wananchi wake, alisema ni mawasiliano ya barabara zinazounganisha wilaya hiyo na maeneo mengine na umaskini. Barabara nyingi zenye matatizo ni za mkoa na taifa.
Alizungumzia barabara ya Kagoma-Lusahunga ambayo mkandarasi alisimamishwa na serikali, lakini haijatangaza hatua dhidi ya waliOmpatia zabuni wakati hana uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Yeye binafsi anapambanaje na maisha baada ya kutenguliwa kwa ubunge wake? “ Kwa sasa mimi ni mkulima. Ninalima mahindi na pia nina shamba la migomba. Hivyo ndivyo vyanzo vyangu vya mapato kulipa madeni na hasa mkopo wa bunge. Kuna miezi inapita bila kulipa.”
“Nilipovuliwa ubunge, hata kwenye Bunge la Afrika sikwenda tena. Kwa dhamira safi niliacha kwenda. Ukiendelea huo ni ufisadi kama ufisadi mwingine, maana ubunge huo wa Afrika niliupata kupitia bungeni.
Kuhusu hali ya kisiasa wilayani Biharamulo na kwenye chama chake cha siasa, mzee huyo alisema: “Huo mgawanyiko unaosikia huko juu hapa haupo. Sisi tunashirikiana kama kawaida. Tuna ushirikiano wetu na mwenyekiti wetu wa wilaya ni Martini Raphael wa Chadema.
Mzee huyo ambaye alieleza nia yake ya kuhudhuria mkutano Mkuu wa Tanzania Labour Party (TLP) unaotarajiwa kufanyika kesho, alidokeza nia yake ya kuwania tena nafasi ya Umakamu Mwenyekiti (Bara) na ujumbe wa Halmashauri Kuu (seneti) alizokuwa anashikilia kabla ya kifo chake.
Hata hivyo alikuwa makini kuzungumzia mgogoro kati ya Mwenyekiti wa TLP anayemaliza muda wake Augustino Mrema na baadhi ya wanachama wake kuhusu uchaguzi wa kesho:
“Chama si mtu; Mrema anaweza kutofautiana na baadhi ya wanachama au wanachama wakatofautiana na chama kikaendelea. Migogoro ya sasa siwezi ‘kucomment, sikuwapo, sijui sababu ya ugomvi wao, sijaongea na Mtungirehi wala Mrema,” alisema.
Baada ya mazungumzoa hayo tuliagana na nami nikaondoka, nikitarajia kuchapisha mahojiano nifikapo Dar es Salaam baada ya mapumziko yangu. Baada ya siku tatu, nikiwa mjini Bukoba, Mzee huyo alinipigia simu tena akitaka nirejee kwake, kwa sababu alikuwa na nyongeza ya mazungumzo.
Nilipanga naye miadi na tulipokutana, alinieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha serikali wilayani humo kuwataka wananchi wa kitongoji cha Isesa Maharage, kijiji cha Lusahunga wahame kupisha eneo la mgodi wanalodaiwa kuvamia.
“Mkuu wa wilaya amewataka wananchi wote wahame. Wengine wamekaa muda mrefu na wamefuata taratibu zote za kuishi hapo, mimi sioni sababu ya kuwahamisha wote, wangefanya uchunguzi na kubaini nani wa kuhama na nani ana haki ya kukaa hapo,” alisema.
Jana, baada ya kuripoti ofisini na kuanza kuandaa mnakala yake, nilipata taarifa za kifo chake, kutokana na ajali ya barabarani iliyomkuta akielekea jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo wa TLP. Bwana ametoa, bwana ametwaa, jina lake linarikiwe
1 comment:
Story ya kuuzunisha kabisa.... Mungu aliaze roho ya marehemu Kabuye mahala pema.
Post a Comment