Sunday, November 28, 2004

RSM Sasa Nataka Ubunge

NIMEFIKIRIA kwa muda mrefu na kubaini jambo moja ninalohitaji. Jambo lenyewe si jingine bali ni kuwania ubunge. Nataka kuwa mjumbe katika Bunge Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hapa Dodoma.

Tangu Novemba 2003 nilipowasili mkoani hapa na kuanza kuripoti habari za Bunge, nimekuwa naingia katika kijisehemu wanapokaa waandishi wa habari, maarufu kama Press Gallary. Bila utani mle ndani ni kama lupango. Kuna ulinzi wa hali ya juu wa watu; na wa mitambo. Huwezi kuingia na kitu chocote asili ya chuma, mtambo utapiga 'filimbi' na utakaguliwa vilivyo.

Ukiwa mle ndani wabunge unachungulia kwa mbali kwenye vioo, huwezi kuwafikia. Utawafikiaje bila ruksa maalum ya Spika wa Bunge ya kukanyaga zuria jekundu?

Ukiwa ndani ya hivyo vioo unaweza kusikia vizuri yanayoelezwa buneni kupitia kinasa sauti kimoja kilichowekwa kwenye Press Gallery. Hapo utasikia sawasawa jinsi wabunge wanavyoitana WAHESHIMIWA.

Sina uhakika kama nataka ubunge ili ama niitwe
mheshimiwa au niruhusiwe kukanyaga zuria jekundu. Lakini uhakika nilionao ni kuwa sitaki kuendelea kuwachungulia waheshimiwa kwenye vioo bali nataka niwe nao ndani ya ukumbi, nitunge nao sheria.

Nataka nikae humo ndani hata kama sina cha kuchangia katika miswada ya sheria au mijadala mbalimbali itakayofanyika. Hata kama sitakuwa nasikiliza chochote, hata kama sitamwakilisha mtu yeyote, niwemo tu bungeni kama walivyo wengine?

Nikiwa ndani ya bunge nikijiwakilisha mimi na familia yangu, nitafanya mambo mengi ya kibinafsi na kuigiza mengine wanayofanya wabunge wenzangu; baadhi yake ni haya;

Mosi, Nitashangilia sana yanayozungumzwa kwa kugonga meza hata kama sijasikia kilichozungumzwa.

Pili, nikishachukua 'bahasha' za mshiko wangu wa kukaa 'siting allowances' naondoka hadi siku inayofuata.

Tatu, Nitamkemea yeyote anayetaja jina langu bila kuanza na neno 'Mheshimiwa'.

Nne, nitaweza kusimama bungeni na kusema lolote. Au niwe tu mchekeshaji wa bunge kwani haitajiki?

Tano, kikubwa hasa nataka niuzindue ukumbi mpya wa bunge ambao tayari umeanza kujengwa hapa Dodoma.

Lakini wakati huo sitafanya mambo yafuatayo;

Mosi, wakati wa kuchangia hoja sitawaangalia waandishi wa habari kuhakikisha kama wananukuu ninachozungumza.

Pili, sitawaandikia kimemo waandishi/wapigapicha kuomba 'wanione' kwenye kamera au maandishi yao.

Tatu, Sitakuwa nakosa kikao chochote, isipokuwa nitakuwa naondoka mapema.

Hizo ndio sera zangu,mwenye mawazo zaidi aniongezee ili niweze kuchanguliwa hapo mwakani.

NAOMBA KURA ZENU. Hata msiponipigia kura nitashinda tu, kwani namba ya wabunge inaongezeka, wabunge wapya watatoka wapi kama si mimi, pia, nimeshakusanya vimilioni kadhaa (miwani) nikiwagawia wenye njaa wataweza 'kuona' jina langu kwenye karataza kupigia kura.
Alamsiki







No comments:

Post a Comment