Saturday, November 27, 2004

Mvua ya Nguvu Dodoma

Nov 27

Na Reginald Simon, Dodoma

MSIMU wa mvua mkoani Dodoma umeanza jana kwa rekodi ya
milimita 90.4 za mvua, kiwango ambacho hakijapata
kutokea kwa miaka miwili mfululizo.

Mvua hizo zilinyesha kuanzia juzi jioni na kuendelea
jana asubuhi, na kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
(TMA) Kanda Kati, mvua hizo zingeendelea kwa kiwango
hicho kwa saa 48, na baadaye kwa viwango tofauti
kutegemeana na hali ya pepo zenye unyevunyevu.

Kaimu Meneja wa Kanda wa TMA, Hamad Mahundi,
alilieleza Mwananchi Wiki Hii kuwa kiwango hizo cha
mvua hakijafikiwa mwaka huu na mwaka 2003, kiwango cha
juu kabisa cha mvua kilikuwa milimita 89.5 iliyonyesha
Desemba 19.

“Kiwango hiki cha mvua si cha kawaida mkoani Dodoma.
Zimeanza kwa kasi mno,” alisema Mahundi, lakini
hakuweza kueleza kama mvua hizo zingeweza kusababisha
maafa au la.

Katika maeneo kadhaa ya mji wa Dodoma mji ya mvua
yalifurika barabara kutokana na mifereji yake kuzibwa
na takataka na katika barabara ya Kikuyu
inayojengwa,baadhi ya mifereji iliziba kwa mchanga na
kuhitaji kuchimbwa upya.

Mahundi aliwashauri wakulima kuanza kuandaa mashamba
na kupanda mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na
yanayostahimili ukame kwa kuwa mvua za mwaka huu
zinatarajiwa kuwa za wastani.

Alisema endapo popo zilizosababisha mvua hiyo
hazitabadilika, mvua za msimu huu zitaendelea kuwa
kubwa hadi katikati ya Desemba.

Mwisho

No comments:

Post a Comment