Thursday, November 25, 2004

Maji kibao Dodoma, hayafiki kwa wanywaji

Nov 21

Na Reginald Simon, Dodoma

LICHA ya Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dodoma
(DUWASA) kuzalisha maji ya kutosheleza mahitaji ya
mjini huo bado haijaweza kufikisha maji hayo kwa
wakazi wote.

Hayo yamebainika mwishoni mwa wiki, wakati wa ziara ya
baadhi ya wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa mamlaka
kadhaa nchini katika visima na pampu za kusukuma maji
zinazomilikiwa na mamlaka hiyo.

Wageni hao walifanya ziara hiyo ili kupata uzoefu wa
DUWASA baada ya mkutano wao uliotishwa na Wizara ya
Maji na Maendeleo ya Mifugo ili wafahamiane, wajadili
wajibu na mwelekeo wa mamlaka zao katika utandawazi.

Katika ziara hiyo, wageni hao walifahamishwa kuwa
mamlaka hiyo inazalisha maji katika visima 21
vilivyopo katika Bonde la Makutopora lakini maji
yanayosambazwa ni ya visima vinane tu, ingawa wakazi
wengi wa mjini Dodoma hawajafikiwa na huduma hiyo.

Wageni hao kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Rukwa, Iringa,
Babati walionyeshwa jinsi mji wa Dodoma unavyopanuka
kwa kasi wakati mamlaka hiyo inashindwa kuwafikishia
huduma ya maji.

Katika eneo la Ipagala, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA,
Mhandisi Peter Mokiwa, alisema kuna ongezeko la nyumba
mpya 110, zinazojengwa 87 lakini zote hazijapata
huduma ya maji licha ya kumilikiwa na watu wenye uwezo
wa kuingiza na kulipia maji.

“Kwa ujumla katika kuna zaidi ya nyumba 1,000 mpya za
ambazo hatujaweza kuzipatia huduma ya maji,” alisema
Mokiwa.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, mamlaka hiyo
imeamua kukopa sh milioni 200 kutoka benki ya CRDB
kupanua mtandao wa maji ili kuwafikia watu wengi
zaidi.

DUSAWA, sawa na mamlaka nane za daraja A nchini,
inajiendesha kwa asilimia 100 lakini tofauti na
wenzake, inatumia maji ya visima kutoka mita 150
nchini ya ardhi na umbali mrefu kutoka mjini Dodoma,
hivyo kuhitaji umeme wa gharama kubwa na watumishi
wengi.

mwisho

No comments:

Post a Comment