Matokeo ya uchaguzi huu yanadhihirisha kuwa ili upinzani uweze kushinda viti vingi zaidi vya ubunge, kazi ya ziada inahitajika. Si sahihi kudhani/kushutumu wananchi kwa kufanya uamuzi wao wa kidemokrasia katika kuamua nani awe mwakilishi wao. Wameamua kuipa CCM nafasi hiyo, na hiyo ni haki yao na ni sahihi kabisa.
Ni sahihi pia kama wangeamua mgombea mwingine yeyote kuwa mwakilishi wao Bungeni. Wao ndio wanaojua wanachokitaka, na wamechagua wanachokitaka.Wapinzani na hasa CHADEMA ni vyema wakafahamu kuwa, kura walizopata zimetokana na kazi nzuri waliyofanya Busanda. Tunatakiwa kufahamu kuwa 2010, kura hizo zinaweza kuongezeka ama kupungua, kutokana na jinsi watakavyoamua kuzilinda na/au kuziongeza.
Kwa mtazamo wangu, wapinzani wanatakiwa kufanya yafuatayo ili kujihakikishia ushindi katika chaguzi zifuatazo;
1. Wahakikishe wanakuwa na matawi mengi vijijini: Wananchi wa vijijini hawana kitu kinachoweza kuwafanya waamini kuwa wapinzani wanaweza kuwaletea mabadiliko wanayoyahitaji. Bila vyama vya upinzani kuwa na presence kubwa vijijini, chaguzi mbalimbali zitaendelea kuwashangaza.
2. Wahakikishe kuwa, sera zao zinalenga katika kujibu matatizo ya hali halisi ya wananchi wanaotarajia kuwaomba kura. Sera ziwekwe bayana, na ziwe zinazokubalika. Kubainisha mapungufu bila kutoa suluhu ya matatizo, haimaanishi kuwa matatizo hayo yatakwisha endapo wapinzani watachaguliwa. Inabidi kutoa utatuzi wa matatizo hayo na kubainisha jinsi ambavyo sera za CCM haziwezi kuyatatua bali wao pekee ndio wenye uwezo huo.
3. Wahakikishe kuwa mikakati ya ushindi ni endelevu. Wasiweke jitihada za ushindi wakati inapotokea nafasi ya uchaguzi tu. Inabidi hata kipindi ambacho hakuna uchaguzi, kuwe na tathmini zinazoweza kuwafanya wajue idadi ya kura wanazoweza kupata endapo uchaguzi utafanyika, na ubunifu wa mbinu za kuziongeza kura hizo (kata hadi kata). Tathmini hizo ziwe za ukweli na zinazoendelea kubadilika siku hadi siku, wiki hadi wiki, mwezi hadi mwezi na hata mwaka hadi mwaka.
4. Wajue mbinu zinazotumiwa na wapinzani wao. Waangalie nguvu za kila chama katika eneo husika, na watafute mbinu za kuweza kuzishinda nguvu za wapinzani wao kila mara. Wajue pia udhaifu wa wapinzani wao na kuutumia bila subira katika kujenga nguvu zao. Wakati huo huo, wanatakiwa wajue nguvu ya baadhi ya wananchi wenye kukubalika katika maeneo husika, na hao watumike kuongeza nguvu zao.
5. Kampeni ni njia ya kuomba kuchaguliwa au kujenga kukubalika kwa wananchi. Upinzani unatakiwa kujua jinsi ya kuongea na wananchi ili waweze kukubalika kwao. Mbinu za ubabe, matusi au kashfa haziwezi kusaidia kuongeza kukubalika kwa chama chochote. Wananchi huogopa na pia huchukizwa na vyama vinavyotumia nguvu nyingi, dharau na maneno yasiyoonyesha nidhamu katika kuomba kura. CCM imeshinda Busanda, na CCM inaweza kushinda sehemu nyingine nyingi zaidi endapo upinzani utaendelea kutojifunza kutokana na matokeo katika majimbo kama haya (Busanda, Tarime). Kila uchaguzi ni lazima uzae somo kwa wanasiasa wanaokusudia kupata ushindi kwa vyama vyao. Source: Bidiiforum
No comments:
Post a Comment