Friday, March 11, 2005

Mwandishi wa Habari Kuwa Tena Rais wa Tanzania?

INGAWA hana umaarufu mkubwa kisiasa, lakini ni mtu anayejulikana kutokana na kazi zake za uandishi wa Habari. Huyu si mwingine, ni Patrick Chokala, aliyewahi kuwa mwandishi wa Habari wa Marais wawili mfululizo, Ali Hassan Myinyi 'Mzee Ruksa' na Benjamin Mkapa tangu mwaka 1986 hadi 1998.
Amefanya nini? Hajafanya lolote mbali na kuchukua fomu za kuwania uteuzi wa CCM kuwa Mgombea Urais wa Awamu ya Nne. Amefuata taratibu zote, kwa kuonyesha kadi hai ya CCM na kulipia sh 1,000,000. sasa hivi yuko mbioni kutafuta wadhamini wasiopungua 250. Kati yao, angalau kila mkoa, kati ya mikoa isiyopungua 10, miwili ikiwa ya Zanzibar, wapatikane wadhamini 25.
Basi, endapo Chokala atateuliwa kuwa Rais, atarithi kiti cha rais anayemaliza muda wake, Mkapa ambaye pia aliwahi kuwa mwandishi wa habari na mhariri wa Daily News.
Kutokana na maelezo yake binafsi, gazeti la Mwananchi liliandika yafuatayo, katika toleo lake la March 11;

Chokala naye ajitosa kinyang'anyiro cha Urais

Na Reginald Simon, Dodoma

BALOZI wa Tanzania Urusi, Patrick Segeja Chokala (57) amekuwa Mtanzania wa tisa kuchukua fomu za kuwania uteuzi wa kuwa mgombea urais CCM na kujigamba kuwa haogopi wazito waliotangulia kufanya hivyo.

Chokala aliyasema hayo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari na baadhi ya wana-CCM, mara tu baada ya jkukabidhiwa fomu yake na Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, katika makao makuu ya chama hicho mjini hapa.

Alisema umma wa watanzania ni mzito kuliko wazito
waliokwishachukua fomu au wengine watakaochukua,
wakiwa mmoja mmoja, hatakubali kukatishwa tamaa na mtu yeyote.

Alisema, “anayetaka kunikatisha tamaa, awe ni ninyi
waandishi wa habari au mtu mwingine yeyote atakuwa anapoteza muda wake,” alisema.

Akizungumzia rushwa, alisema ni wajibu wa kila
mwanajamii kushiliki kikamilifu katika vita hiyo,
wakiwemo waandishi wa habario ambao ana uhakika nao wamo miongoni mwa wala rushwa.

“Sitaki kuamini kuwa waandishi wa habari mko immune kuhusu rushwa, nyinyi ni sehemu ya jamii na ngoja tuone katika uchaguzi mkuu itakuwaje. Ndugu katibu Mkuu wakati huu wa kampeni ni kipindi cha kumbikumbi wa kuvuna,” alisema Chokala.

Chokala alijigamba kwa kutekeleza vizuri sera mpya ya diplomasia ya uchumi kwa kuitangaza Tanzania kiutalii nchini Urusi ambapo amefanikiwa kuongeza watalii wa Kirusi kutoka kati ya 10 na 20 mwaka 2002 hadi 200 mpaka 300 kila mwezi.

Alisema kuna Warusi wengi wanaokuja nchini sasa kwa shughuli za kibiashara, wakiwemo wanaotaka kujenga kiwanda cha dawa za maji, lakini wakakwamishwa na bei ya umeme, hivyo kuamua kujenga kiwanda cha mitambo ya umemejua.

Akizungumzia ukimwi, Balozi Chokala alisema
angependelea kijengwe kiwanda cha dawa za ukimwi
nchini lakini baada ya kufanya utafiti wa aina ya dawa zinazohitajika.

Pia, Chokala ambaye alishindwa kutaja neno ‘kondom’, alisema elimu zaidi juu ya matumizi ‘hii kitu’
inatakiwa ipelekwe vijijini ambapo wananchi wanadaiwa kuzifua na kuazimana.

Kwa mujibu wa Chokala, Ikulu kwake si mahali pageni, kwani alikuwa msaidizi wa marais wawili na kushiriki mikutano muhimu ikiwemo ya baraza la mawaziri.

“Wakati naongea na waandishi wa habari badala ya Rais Ali Hassan Mwinyi nilikuwa nafanya mazoezi,” alisema.

Vile vile, kwa ufupi, alizungumzia watumishi wa umma wasiowajibika ipasavyo kuwa ‘‘watapata habari yao’’.

Akizungumzia sera ya Rais Mwinyi ya ruksa, alisema
haikuwa na ubaya wowote kwani ilifungua milango ya
biashara huria na mageuzi makubwa kiuchumi, hali
ambayo imeongeza ajira na bidhaa kuongezeka.

Alisema sera hiyo imeendelea hata wakati wa awamu ya nne chiniu ya Rais Benjamin Mkapa na hadi sasa haoni ubaya wake.

Chokala ambaye alikiri kuwa ni mlokole, alisema
serikali yake itaendelea kutumia viwanda vya bia na
sigara kama vyanzo vya mapato ya serikali, kwa kuwa serikali haina dini bali watu wake ndio wenye dini.

Kuhusu vijana kukosa kazi na kukimbilia mijini,
alisema hilo ni bom,u linalosubiri muda wake, lakini
akasema akishika madaraka atavifanya vijiji viwe
mahali pa kuishi, ili vijana hao wasikimbilie mijini.

Chokala mwenye elimu ya chuo kikuu, amefanya kazi kama mwandishi wa rais kwa tangu mwaka 1986 hadi 1998, chini marais Mwinyi na Mkapa, katika Wizira ya Mambo ya Nje ns Ushirikiano wa Kimataifa na katika ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria kama Katibu wa kwanza na mshauri wa balozi.

Pia,aliteuliwa kuwa balozi mwaka 1995 lakini
akaendelea kuwa mwandishi wa rais hadi mwaka 1998 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje kwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Habari, Sera na Mipango, kabla ya kuteuliwa kuwa balozi wa Urusi na nchi zote zilizokuwa chini ya Jumuiya ya Sovieti mwaka 2002.

Katika chama alianza kuwa mwanachama wa TANU Youth League mwaka 1965, baadaye TANU na kuwa mwasisi wa CCM mwaka 1977.


No comments:

Post a Comment